Na Joseph Lyimo
IKIWA ni takribani miaka mitatu tangu janga la UVIKO-19 liingine nchini, wanasayansi wametakiwa kujitathmini ya kuangalia walichojifunza katika kipindi hicho na nini kinaweza kufanyika kama taifa ili kujiandaa dhidi ya majanga.
Janga la UVIKO-19 liliingia nchini mwezi Machi mwaka 2020 na hadi hivi sasa bado kuna wagonjwa wa virusi hiyo hivyo wanasayansi wametakiwa kutathmini uwepo wa UVIKO-19 na kutafuta njia za kukabiliana na majanga.
Mlipuko wa janga hilo umezidi kuthibitisha kuwa kuna umuhimu wa kufanya tafiti katika mifumo ya afya ili kuweka uendelevu wa afya kwa wananchi wote.
Baadhi ya wananchi wanaeleza kuwa inawabidi wataalamu wa afya na wanasayansi kujipanga kikamilifu kwa kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kujipanga kwenye changamoto zinazotokea kama UVIKO-19.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Mashaka Jororo anaeleza kuwa wasomi wanapaswa kutumia elimu yao kwa kuandika maandiko kupitia tafiti ili majanga kama UVIKO-19 yakitokea wananchi wawe wamejiandaa.
Jororo anasema wanasayansi hao na wataalamu wa afya kupitia tafiti hizo zitasaidia mno wananchi kwa miaka ijayo ili kukitokea tena maradhi mithili ya UVIKO-19 jamii ifahamu kuwa inakabiliana nayo kwa namna ipi tofauti na sasa.
“Tunamshukuru hayati Rais wa awamu ya tano John Magufuli kwa kuwatoa hofu wananchi wa Tanzania na kuwajengea uwezo kuwa wasihofu juu ya uwepo wa UVIKO-19 suala ambalo lilichangia wao kuishi na kutokufa kwa hofu,” anasema Jororo.
Mkazi wa kata ya Maisaka Mjini Babati Mkoani Manyara, Abdalah Juma anasema kupitia wataalamu mbalimbali nchi inaweza kunufaika na mifumo ya afya, kupitia tafiti zao.
“Huu ndiyo wakati ambapo wataalamu wetu wa sayansi na kada ya afya, kujipambanua kwenye utaalamu wao na kufaidisha wananchi kupitia tafiti zao za uhakika zenye kuteta tija kwa jamii,” anasema Juma.
Mkazi wa mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, Julius Gapchojiga anaeleza kwamba endapo wataalamu wa afya na wanasayansi wakifanikisha kufanya tafiti na kuja na njia bora zaidi ya kupambana na majanga kama UVIKO-19 itakuwa nafuu kwa wananchi.
“Tunao wataalamu wazuri tuu hapa nchini hivyo wajifungie ndani wafanye jambo kubwa kama hilo kwa kuhakikisha wanatupa njia ya kupita au namna ya kufanya pindi majanga kama UVIKO-19 yakijitokeza,” anasema Gapchojiga.
Mkazi wa kata ya Bwagamoyo Wilayani Kiteto Hamis Jumanne anasema kuwa wanasayansi wakifanya jambo hilo itakuwa nafuu kwao kwani siyo vyema majanga kama UVIKO-19 yanatokea na watu wanashindwa namna ya kupambana nayo kwa haraka.
“Tuna matumaini makubwa na wataalamu wetu kuwa watafanikisha suala hilo na kuhakikisha wanajipanga kutuletea mrejesho ili majanga mengine kama haya yakitokea tuwe tumejipanga tayari,” anasema Jumanne.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea udaktari kwenye chuo kikuu cha Dodoma, Henry Urio anasema suala hilo ni muhimu kwa wataalamu wa sayansi kufanya tafiti mbalimbali na kuja na majibu kupitia maandiko yao.
“Ni wazo zuri katika kuhakikisha mwarobaini wa majanga kama UVIKO-19 pindi yakitokea wananchi wafahamu kuwa wanapambana nayo kwa hali gani kama changamoto ya UVIKO-19 ilivyokuja bila hodi.” anaeleza Urio.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Aifelo Sichalwe hivi karibuni wakati akifungua kongamano la 10 ya kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili lililofanyika jijini Dar es Salaam, ameunga mkono suala hilo.
Anasema kuwa walifanya kongamano lililokuwa limebebwa na kauli mbiu ya mchango wa utafiti kwenye mifumo ya afya katika kuhamasisha na kujenda uendelevu wa afya kwa wote, “Mambo tuliyojifunza kutokana na Janga la Uviko 19.”
Dk Sichalwe anasema kuwa janga hilo lilikuja nchini wakati ambapo mifumo ya utoaji huduma haikuwa stahimilivu hivyo kuna kila sababu ya tafiti nyingi kufanyika ili kuweza kuweka mipango thabiti ya kujiandaa dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
“Janga hili limetupa funzo la kuimarisha mifumo yetu ya utoaji huduma na kuzuia magonjwa, kama kuna ugonjwa unatokea basi tuweze kuchukua hatua na kuutolea tarifa mapema, anasema Dkt Sichalwe.
“Tumejifunza pia dhana nzima ya utoaji huduma katika milipuko na ndiyo maana tulipopata ule mkopo wa IMF hatukwenda kununua barakoa bali tulitengeneza miundombinu ya afya,” anaeleza Dkt Sichalwe.
Anasema kwamba katika hayo wamefanya kukumbushana wanasayansi kuhusu umuhimu wa kufanya tafiti ili kukabiliana na majanga kama hayo.
“Upande wetu kama Serikali tutaendelea kuwawezesha ili tafiti nyingi zifanyike ambazo zinatusaidia pia katika maboresho na utengenezaji wa sera, pia tutaongeza uwezo wa wataalam wa afya kwa kuwapatia mafunzo na kuongeza idadi yao,” anasema.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas Profesa Andrea Pembe anasema kuwa lengo lao ni kuwakutanisha wanasayansi waliofanya tafiti mbalimbali kuzijadili kwa pamoja kwa ajili ya kutengeneza matokeo chanya kwa jamii.
“Tukiangalia sasa hali ya afya haipo vizuri, hali za magonjwa zimebadilika kutokana na mtindo wa maisha bila kusahau athari za mabadiliko ya tabia nchi,” anaeleza Profesa Pembe.
“Kwa hivyo sisi kama wataalam tunapaswa kufanya tafiti ili kuweka wazi tunaweza kukabiliana vipi na hali hizo za majanga na milipuko,” anamalizia kwa kusema Profesa Pembe.