MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 29,2022 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Taasisi hiyo kwa Kipindi cha Mwaka 2021/22 na Matarajio kwa Mwaka 2022/23.
WAANDISHI wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo,wakati akizungumzia Mafanikio ya Taasisi hiyo kwa Kipindi cha Mwaka 2021/22 na Matarajio kwa Mwaka 2022/23 leo Julai 29,2022 jijini Dodoma.
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 29,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Mafanikio ya Taasisi hiyo kwa Kipindi cha Mwaka 2021/22 na Matarajio kwa Mwaka 2022/23.
………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA kwa kipindi cha mwaka mmoja imefanikiwa kukamata na kuteketeza bidhaa za dawa na vifaa tiba bandia na visivyokidhi ubora jumla ya tani 35.54 elfu zenye thamani ya shilingi bilioni 35.53 ambazo bila udhibiti zingeingia sokoni na kutumiwa na binadamu.
Hayo yamesemwa leo Julai 29,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Bw. Adam Fimbo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo amesema wataendelea kudhibiti dawa bandia zinazoingizwa hapa nchini na kuwataka wanaofanya hivyo kuacha mara moja.
Amesema,ili kulinda afya za walaji, TMDA imekuwa ikifuatilia,kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora,usalama na ufanisi ili kuepusha zisitumiwe na kwamba mpango wa ufuatiliaji wa ubora wa bidhaa katika soko hutumika wakati wa ufuatiliaji huo.
”Katika kuteketeza bidhaa zisizofaa Kwa matumizi, katika mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi na thamani ya bidhaa za dawa na vifaa tiba visivyofaa zilizoteketezwa imeongezeka kutoka tani 14,704.80 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.5 hadi kufikia tani elfu 35,547.47 zenye thamani ya bilioni 35.53 ambazo ziliteketezwa kwa mwaka 2021/22.”amesema Bw.Fimbo
Bw.Fimbo amesema kuwa bidhaa hizi zinajumuisha bidhaa zilizotolewa taarifa na zile zilizokamatwa katika kaguzi mbalimbali ambapo kuongezeka kwa bidhaa zilizoteketezwa Kutokana na kuimarisha ukaguzi na elimu kwa umma inayosaidia wateja kutoa taarifa juu ya bidhaa zisizofaa Kwa matumizi.
Akielezea mpango mkakati wa kitaifa wa miaka mitano 2021 hadi 2026 wa kupambana na tumbaku pamoja na mpango kazi wa miaka mitano wa udhibiti wa tumbaku, mkurugenzi mkuu huyo wa TMDA amesema mfumo wa udhibiti wa bidhaa hizo na hadi sasa wamekwisha tambua bidhaa zote za tumbaku zilizoko kwenye soko ambapo idadi yake ni bidhaa 51.
Aidha,Fimbo amesema kuwa kwa sasa mamlaka hiyo imeanzisha maabara ya upimaji wa bidhaa za tumbaku kwenye jengo lake lililoko jijini Dodoma.
Kuhusu ukaguzi wa Viwanda 15 vya dawa (8 vilivyosajiliwa na 7 vipya) ndani ya nchi vilikaguliwa ambapo viwanda viwili (2) kati ya 7 vipya vimekidhi vigezo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni. Hili Ni ongezeko la viwanda 6 sawa na 67% ikilinganishwa na viwanda 9 vilivyokaguliwa mwaka 2020/21.
Aidha, jumla ya viwanda vipya 21 vya vifaa tiba vilisajiliwa ikiwa ni ongezeko la viwanda 18 ikilinganishwa na viwanda vitatu (3) vilivyosajiliwa mwaka 2020/21. Hadi kufikia mwezi Juni 2022 jumla ya viwanda 17 vya dawa, 26 vya vifaa tiba na 6 gesi tiba vimesajiliwa na kuanza kufanya kazi.
Moja ya majukumu ya TMDA ni pamoja na kusajili bidhaa za dawa,vifaa tiba na vitendanishi, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, mamlaka hiyo imesajili jumla ya bidhaa 1,286 ambapo kati yake bidhaa za dawa za binadamu na mifugo ni 933 huku vifaa tiba na vitendanishi vikiwa ni 353 na hivyo kufanya idadi ya bidhaa zilizosajiliwa kufikia 8,831 hadi sasa.