Ndugu waandishi wa habari, kila mwaka tarehe 30 Julai ni siku ya kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu. Usafirishaji haramu wa binadamu ni kitendo cha usafirishaji haramu wa binadamu na ni haramu kwa sababu kimekatazwa na sheria za kimataifa hususani zile ambazo zinazotetea na kulinda haki za binadamu. Kubwa zaidi sheria yetu ya kuzuia na kupambana na uhalifu wa aina hii “The Anti-Trafficking in Persons Act, No. 6, 2008 imeharamisha matendo yote yenye viashiria vya usafirishaji wa binadamu wenye lengo la kumtumikisha binadamu kwa kiunyonyaji na ikiwa ni pamoja na kumtendea matendo yanayokiuka haki zake kama binadamu.
Ndugu waandishi wa habari, usafirishaji haramu wa binadamu ni muendelezo wa biashara ya utumwa na hujulikana kama utumwa mambo leo. Usafirishaji haramu wa binadamu ulianza mwishoni mwa karne ya kumi na nane na kushamiri zaidi mwanzoni mwa karne ya kumi na tisa katika baadhi ya nchi za bara la ulaya. Sababu za kushamiri kwa biashara hii ni:-
Mosi, mahitaji makubwa ya nguvu kazi ambayo si ya gharama na inayopatikana bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali.
Pili Kuibuka kwa soko la ngono katika baadhi ya nchi duniani ambalo linahitaji sana wanawake na wasichana.
Tatu ni kuibuka kwa soko la viungo vya binadamu duniani kama vile figo kutokana na baadhi ya watu wenye utajiri kuumwa malazi ya figo. Vile vile viungo vya binadamu vinahitaji katika ushirikina watu wakihitaji utajiri wa haraka haraka.
Mwaka 2021 kulikuwepo na tukio la kuwahusisha watoto 14 waliokolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya wakiwa wanaenda kutumikishwa kazi ya kuchunga Mifugo huko Wilaya ya Mbarali.
Lakini vile vile watu wanasafirishwa kwa ajili ya kwenda kutumikishwa katika vitendo vya uhalifu kama vile kuuza madawa ya kulevya na wenginie kupelekwa kufundishwa uaskari wa kusaidiana na wanajeshi waasi kama kule Kongo na Msumbiji.
Taarifa nyingi za kimataifa zinaonesha kuwa usafirishaji haramu wa binadamu ni biashara ya tatu hapa duniani inayowapatia faida kubwa sana wahalifu ikitanguliwa na Biashara ya utengenezaji na uuzaji wa Silaha na Madawa ya kulevya.
Ndugu waandishi wa habari, usafirishaji haramu wa binadamu huenda sambamba na mateso makubwa kwa watu ambao ni wahanga wa uhalihu huu. Mateso hayo ni kama vile kupigwa, kubakwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi bila malipo, kunyang’anywa hati zao za kusafiria, kuuzwa kwa waajiri zaidi ya mmoja, kufanyishwa kazi bila mapumziko, kulazimishwa kutoa mimba, na wengine kupata mateso na pia kuuwawa au kuamua kujiuwa wenyewe.
Ndugu waandishi wa habari, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai, 2022 jumla ya raia wa kigeni 169 kati yao raia wa nchini Ethiopia 97, Somalia 37, Burundi 07, Rwanda 21, Kenya 02, Uganda 01, Congo 02, Malawi 01 na Angola 01 walikamatwa wakiwemo watoto wakisafirishwa kwenda nchi za jirani.
Aidha kwa kipindi hicho, jumla ya magari 11 yamekamatwa yakitumika kusafirisha wahamiaji haramu ambayo ni:-
- T.888 CRM Toyota Land Cruiser V8
- T.154 DMF Toyota Land Cruiser V8
- T.122 BMV Toyota Noah
- T.902 DFS na Tela Na. T.983 BNT Benz Lori
- T.497 ARB Toyota Mark II
- T.564 BDG Toyota Mark II
- T.648 BES Toyota Brevis
- T.386 CWG Mitsubish Dion
- T.309 ANX Fuso Lori
- T.139 BSE Toyota Super Custom
- T.423 BAK Toyota Mark II.
Aidha katika kipindi hicho, jumla ya mawakala wa usafirishaji wahamiaji haramu 07 wote raia wa Tanzania wamekamatwa ambao ni:-
- ANGELILE NASSON [43] Mkazi wa Kyela.
- BROWN LARISA [46] Mkazi wa Dar es Salaam
- AUGUSTINO MICHAEL [40] Mkazi wa Jijini Mbeya
- HEMED ABEID [46] Mkazi wa Mkoani Tabora
- MANENO KUJOKWA [27] Mkazi wa Kyela
- PAUL NORBERT MWAMKONGA [47] Mkazi wa Mkoani Iringa
- KURWA NGORO [35] Mkazi wa Makambako.
HATUA AMBAZO JESHI LA POLISI LIMECHUKUA KUPAMBANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMUI HAPA NCHINI.
- Kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojihusisha na biashara hii.
- Kuongeza juhudi za kuelimisha jamii ili ipate uelewa wa madhira wanayoyakuta wanawake, wasichana, watoto na vijana waodanganywa kwenda kufanya kazi ndani au nje ya nchi bila kufuata taratibu za kisheria.
- Kufanya ukaguzi na utambuzi wa wahanga maeneo ya viwanja vya ndege.
- Mtakumbuka kuanzia Julai 13 hadi 15, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Beaco yalifanyika mafunzo maalum ya kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu, mafunzo ambayo yalihusisha maafisa kutoka ofisi ya Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Tanzania Relief Initiatives, maafisa kutoka Jeshi la Polisi, Magereza na Uhamiaji, Idara ya mahakama na ustawi wa jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo na weledi katika utendaji kazi.
Wito: Wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za kuwafichua mawakala wa usafirishaji wahamiaji haramu kwani wengi wao ni wakazi wa maeneo yao na wanawajua. Pia wananchi waendelee kutoa taarifa pindi waonapo watu au kikundi cha watu wanachokitilia mashaka ili hatua za haraka zinafanyike ikiwemo ya kuwakamata kwa ajili ya upelelezi na kujiridhisha juu ya uraia wao.
Imetolewa na:
Ulrich O. Matei – SACP
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya.
Jiandae kuhesabiwa siku ya jumanne tarehe 23 Agosti, 2022.