Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida limewakutanisha
madereva wa bajaj na,pikipiki kwa lengo la kuwaomba kuwa mabalozi wao
ambao watakuwa wakitangaza huduma zinazotolewa na shirika hilo.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Rehema
Mwaipopo, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na madereva hao katika Ukumbi
wa Vatican uliopo eneo la Mwenge mjini hapa.
Alisema wameamua kushirikiana na madereva hao kutokana na uwingi wao na
huduma wanazozitoa ambapo kila siku wanakutana na watu jambo ambalo litasaidia
kwa kiasi kikubwa kutangaza huduma za Tanesco.
Mwaipopo alisema hao watawaunganisha katika mfumo ambapo
watakuwa wakipata ujumbe kwenye simu zao ambao utakuwa na taarifa mbalimbali
zikiwamo za kukatika kwa huduma na umeme na wao watawajulisha wateja wanao wabeba.
Alisema pamoja na mambo mengine aliwataka madereva hao kutoa taarifa
mbalimbali pale wanapoona matukio ya kuharibu miundombinu ya shirika
hilo katika maeneo wanayopita.
“Kumekuwa na tabia ya watu wasio waaminifu kung’oa vyuma kwenye nguzo za
umeme mkubwa kwa ajili ya kutengenezea mikokoteni ya kukokotwa na ng’ombe na
matumizi mengine kama kutengeneza mapanga na zana nyingine mkiona uharibifu huo
tupeni taarifa kupitia namba zetu tulizo wapa” alisema Mwaipopo.
Aidha Mwaipopo alisema msimu wa kilimo unapoanza kumekuwa na kazi ya
kusafisha mashamba ambayo yapo chini ya nguzo za umeme hivyo wakati wa kazi
hiyo wananchi wanatakiwa wasichome moto kwani wanaweza kusasabisha hatari hivyo aliwaomba madereva hao pindi watakapoona jambo hilo
watoe taarifa.
Pia Mwaipopo aliwataka madereva hao kuwa mabalozi wa kutoa maelezo kwa
watumiaji wa vyombo vya mto kutoegesha vyombo vyao chini ya nguzo za umeme na
transfoma kwani kunaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na vyombo hivyo vya moto.
“Ninyi sasa ni mabalozi wetu jambo lolote mtakaloliona haliko sawa huko
mnakoishi na kupita linalohusu sekta ya umeme tujulisheni pia kama kutakuwa
hakuna matumizi ya vifaa vinavyotumia umeme kama pasi,majiko, majokofu, taa na
vingine mvizime pia waambieni na wananchi wengine mnaoishi nao na wale
mnaowabeba kwenye vyombo vyenu”alisema Mwaipopo.
Aidha katika mkutano huo Mwaipopo alielezea huduma mpya ya maombi ya
kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT i ambayo inafanyika
kwa kutumia simu huku muombaji akiomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika
hilo ambapo aliwaomba mabalozi hao kwenda kuielezea kwa wananchi wanaoishi nao
na wale wanaowachukua katika vyombo vyao vya usafiri.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Wamiliki Pikipiki na Bajaj Tanzania (CHAMWAPITA)
Mkoa wa Singida, Ahmed Mohamed alitumia nafasi hiyo kulishukuru shirika hilo
kwa kufadhili mkutano na kuratibu mpango huo ambao ni muhimu kwa wananchi
ambapo kama mabalozi ameahidi watatoa ushirikiano wa hali na mali ili kufikia malengo.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani hapa limekuja na mikakati ya
kuboresha huduma zake ambapo madereva wa bajaj na pikipiki watakuwa
mabalozi wa kutangaza shughuli zinazofanywa na shirika hilo kwa wateja wao
wanaowachukua.
Mikakati hiyo mipya imekuja baada ya Tanesco Mkoa wa Singida kupata Meneja
mpya Mhandisi Florece Mwakasege aliyehamishiwa mkoani hapa hivi karibuni
akitokea Mkoa wa Ruvuma.