*****************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini Dkt Dotto Biteko ameruhusu madini ya Ulanga maarufu kama madini ya Kinywe yachakatwe ndani ya eneo tengefu la machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Dkt Biteko akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite amesema siyo jambo jema kuacha madini ya kinywe yazagae na kuonekana uchafu kwa kuhofia wizi wa madini ya Tanzanite.
Amesema kamati ya ukuta wa Tanzanite wanapaswa wajipange kwa kuhakikisha kunawekwa uzio kwenye eneo la kiwanda na kuweka ulinzi madhubuti ili hofu ya wizi isiwepo.
Amesema madini ya kinywe ni utajiri mkubwa duniani siyo vyema wakiwa machimboni kusimama kwenye vifusi vyake pindi wakifanya mkutano ili hali kuna mwekezaji anayahitaji.
“Madini ya kinywe hivi sasa yana soko kubwa duniani, endapo ametokea mwekezaji anataka ayafanyie kazi ni jambo zuri kwani atasababisha mazingira masafi eneo hili,” amesema Dkt Biteko.
Afisa madini mkazi wa Mirerani (RMO) Fabian Mshai amesema wameanza kuratibu mchakato wa kuanzishwa kwa kiwanda ndani ya ukuta unaozunguka madini ya Tanzanite.
RMO Mshai amesema mwekezaji ameonyesha nia ya kuweka kiwanda cha kuchakata masalia ya miambataka yanayozalishwa migodini ndani ya eneo tengefu la machimbo hayo.
“Mwekezaji huyo anaeneo lake tayari lina uzio na atazungumza mwenyewe na wamiliki wa migodi ya Tanzanite ili apatane nao kama watampa kwa gharama gani au atawasafishia mazingira, hayo watapatana wenyewe,” amesema RMO Mshai.