**************************
Julieth Laizer,Arusha
Arusha.Tanzania imekuwa Mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa 3 wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa nchi zinazozalisha Almasi Afrika (ADPA) ambapo itakuwa na mkutano wa Baraza la Mawaziri kesho julai 29 ,2022 katika kituo cha mikutano cha kimataifa Cha Arusha.
Hayo yamesemwa Leo julai 28 jijini Arusha na Waziri wa madini,Doto Biteko wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo.
Biteko amesema kuwa,kikao hicho kinatanguliwa na kikao cha kamati ya wataalamu kinachokaa leo kupitia taarifa na nyaraka na kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza .
Biteko amesema kuwa, mkutano huo pamoja na mambo mengine ni kuidhinisha nyaraka muhimu za ADPA zilizofanyiwa marekebisho ambazo ni katiba,kanuni na miongozo ya umoja huo,na kuteua viongozi watatu(3) wa sekretarieti ambao ni Katibu mtendaji na manaibu wake wawili (2).
“Jumuiya ya wazalishaji wa Almasi Afrika (ADPA) ilianzishwa kwa mujibu wa Azimio la Luanda,Angola,mnamo novemba 2006 ,ambapo lengo kuu la kuundwa kwa ADPA,ni kuzipatia nchi zinazozalisha Almasi Afrika jukwaa la kuzikutanisha nchi zote za Afrika katika kusudi moja la kuhakikisha rasilimali za madini hayo zinanufaisha nchi wanachama “amesema Biteko.
Ameongeza kuwa, Tanzania ilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa baraza la Mawaziri la ADPA kwa mwaka 2021 kwa kipindi cha miaka miwili ,hivyo wanatarajia kukabithi uenyekiti kwa Jamhuri ya Zimbabwe machi 2023,ambapo makabithiano rasmi ya Uenyekiti yatafanyika katika mkutano wa nane wa kawaida wa Baraza la Mawaziri wa nchi zinazolisha Almasi Afrika (ADPA) utakaofanyika katika jiji la Victoria Falls nchini Zimbabwe machi 2023.
Biteko amesema kuwa, ADPA inajumuisha nchi 18 ambapo 12 ni wanachama na 6 ni waangalizi ,ambapo nchi wanachama ni Angola Botswana, Cameroon,Jamhuri ya Afrika ya kati, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,Ghana ,Guinea,Namibia,Sierra Leone,South Africa, Tanzania,Togo na Zimbabwe,huku nchi waangalizi wakiwa ni Algeria,Jamhuri ya Kongo (Brazaville),Gabon ,Ivory Coast,Liberia ,Mali na Mauritania.
Biteko amesema kuwa, kipindi hiki ambacho Tanzania ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo imekuwa ni heshima kubwa kwa nchi kuwajibika kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu hususani katika usimamizi wa madini ya Almasi,ambapo wamewezesha kupitiwa upya kwa mifumo ya jumuiya hiyo ikiwemo marekebisho ya katiba,kanuni na miongozi mbalimbali ya jumuiya .