Taarifa inatolewa kwa wanachama wote wa CCM, walio na nia na sifa za kuweza kugombea na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwamba, mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za maombi ya kuteuliwa kugombea nafasi hizo kupitia CCM, utaanza tarehe 1 Agosti, 2022 na kumalizika tarehe 10 Agosti 2022. Fomu hizo zitachukuliwa na kurejeshwa katika Ofisi za CCM zifuatazo, kuanzia saa 2:00 Asubuhi hadi saa 10:00 jioni :-
1) Makao Makuu ya CCM – Dodoma
2) Afisi Kuu ya CCM – Zanzibar
3) Ofisi Ndogo ya CCM – Dar Es Salaam.
Sifa za mtu anayestahiki kugombea nafasi hizo kupitia CCM, ni kama zifuatazo:-
(a) Awe ni Mwanachama hai wa CCM.
(b) Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(c) Awe na sifa zinazostahiki kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
(d) Awe sio Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mjumbe wa Barraza la Wawakilishi, Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
(e) Awe sio mtumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(f) Awe na uzoefu uliothibitishwa au moyo wa kupenda kuimarisha na kuendeleza malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za maombi ya kuteuliwa kugombea nafasi hizo, ni tarehe 10 Agosti, 2022, Saa 10:00 Jioni.