Na Kija Elias, Moshi
SERIKALI kwa kushirikiana na
wahisani wa Lions Club of Moshi Kibo pamoja na Lions club of Belgium wamekabidhi Chuo cha Ufundi Stadi (VTC) kwa
shule ya watoto wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) Msandaka, iliyopo Manispaa ya
Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza jana katika hafla fupi ya kukabidhiwa kwa chuo hicho,
Mkurugenzi anayeshughulikia watoto wenye mahitaji maalumu kutoka Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Magreth Matonya, alisema chuo hicho ni cha
kwanza kitaifa ambapo hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni mikakati ya serikali
kuhakikisha watu wenye mahitaji maalumu
wanapata ujuzi utakao wawezesha kujikwamua kiuchumi.
Katika hotuba yake Dkt. Matonya aliwashukuru wahisani kwa mchango mkubwa
walioutoa kufanikisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka, kwani kuna
watoto viziwi wanaofikishwa shuleni wakiwa na umri mkubwa ambao hawawezi
kuingia madarasa ya kawaida, wanatakiwa kwenda kwenye madarasa ya ujuzi, kwa
hiyo wakifika shuleni serikali inawabaini na kugundua ujuzi walionao baada ya
hapo wanawapeleka kwenye madarasa ya ufundi.
“Tumekuta wanafunzi hawa wanajifunza ufundi cherehani, wanajifunza ufundi
seremala na ushonaji, tumeona wanatengeneza viti vizuri, stuli nzuri lakini
wana vifaa vya kisasa ambavyo wamepewa na wahisani kutoka Lions Club International,
kituo hiki ni muhimu sana,” alisema Dkt. Matonya.
Aidha Dkt. Matonya alisema uwepo wa chuo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya
shilingi mil. 700 utaifungua jamii kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kwa
kuwa wapo watoto viziwi ambao hawawezi
kufuata mifumo ya elimu ya kawaida, elimu ambayo ni ya mfumo rasmi,
hivyo uwepo wa chuo hicho cha ufundi
utawawezesha watoto hao kupata ujuzi utakaowasaidia katika suala la
kujikimu kimaisha pindi watakaporudi
majumbani.
Dkt. Matonya aliongeza kuwa wapo watoto
wengine waliomaliza kidato cha nne na hawakufanya vizuri lakini wamejiunga na chuo hicho
cha ufundi na wanajifunza kwa bidii na hivi sasa wanafanya vizuri.
Sambamba na hilo Dkt. Matonya aliwashukuru wahisani kwa kutengeneza mabweni
ya kuishi kwaajili ya watoto viziwi
kutokana na mazingira hatarishi ambayo watoto hao wanapitia.
“Kunavitu vingi sana wanavyokumbana navyo wanapokua njiani kuja
shuleni, lakini pia zipo familia ambazo bado haziwajali watoto wenye mahitaji maalum kiasi kwamba
wanawanyanyapaa na kuwaficha, lakini wanapokua bweni wanakua na muda mrefu wa kujisomea kuliko wanapokua nje na shule,”alisema Dk. Matonya.
Mkuu wa shule ya Viziwi Msandaka Rosada Shayo, alisema sababu kubwa ya
kuanzisha ujenzi wa chuo hicho ni baada ya kubaini kuwa wanafunzi wao
wanapomaliza shule ya msingi na kujiunga na sekondari wanapofika kidato cha
pili hurudishwa nyumbani kutokana na matokeo mabaya hivyo kuangukia tena katika
changamoto.
Awali akitoa taarifa juu ya ujenzi
wa Chuo hicho cha Ufundi Stadi (VTC) Mwenyekiti wa Lions Club of Moshi Kibo
Sarah Mandara, alisema ujenzi wa chuo hicho umegharimu kiasi cha shilingi
milioni 700 ambazo zimetumika
kukamilisha ujenzi huo uliojumuisha
vyumba sita vya madarasa pamoja na karakana kwaajili ya watoto kujifunzia.
“Jumuiya ya kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali ya Lions Club of Moshi
Kibo, imefadhili ujenzi wa chuo hiki cha Ufundi Stadi (VTC) katika shule ya
viziwi Msandaka, iliyogharimu kiasi cha
shilingi milioni 700, na leo hii tumekikabidhi kwa Serikali ili watoto hawa
waweze kufikia malengo yao,”alisema Sarah.
Hata hivyo Profesa Jerome Sheridan kutoka Ubelgiji alisema elimu ndiyo kitu
muhimu cha kuwasaidia wenye mahitaji maalum kutokana na changamoto wanazopitia.
“Ndugu wanafunzi, chuo chenu cha ufundi stadi sasa ni halisi, kwanini
tumefanya hivi? kwasababu tuna imani nanyi…licha ya changamoto lakini mnaweza
kuzikabili endapo mtasoma katika chuo hiki,” alisema Prof. Sheridan.
Aidha Profesa Sheridan alisisitiza kuwa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka
kitaenda mbali zaidi ya kujihusisha na kilimo ili kuwajengea uwezo zaidi
wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Kilimo ni muhimu lakini chuo hiki cha ufundi kitaenda mbali zaidi ya
kilimo kwa kuwapatia ujuzi mwingine ili wajitegemee katika maisha yao,” alisema
Prof. Jerome.
Awali Mratibu wa Viziwi Tanzania Selemani Chamshama, alisema miaka ya hivi
karibuni mtazamo wa jamii kuhusu wanafunzi wenye uhitaji maalum umebadilika na
kuwa chanya ukilinganisha na miaka mingi iliyopita.
“Chuo hiki ni adimu kwa nchi yetu. kama mnavyokumbuka miaka ya nyuma jamii
ilikuwa haina uelewa mkubwa juu ya wanafunzi viziwi lakini sasa kumekuwa na
uelewa mkubwa juu ya wanafunzi wenye ulemavu hususani viziwi,” alisema
Chamshama.
Aidha Gavana wa Wilaya wa Lions Club aliyepo Tanzania Mustansir Ghulam Hussein
alitoa shukrani zake za dhati kwa Lions Club wa Ubelgiji kwa kufanikisha ujenzi
wa chuo hicho.
“Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kutuunga mkono, pamoja tumesimama na
pamoja tumeuungana…ndoto tuliyoota pamoja sasa imekuwa halisi,” alisema Ghulam
Hussein.
Kwa upande wake Katibu wa Lions Club of Moshi Kibo, Inderjeet Rehal kwa jina maalufu ‘NITU’ alisema, “Malengo ya
kuanzishwa kwa Chuo cha Ufundi Stadi ni kuwezesha vijana hao wanapomaliza
darasa la saba waweze kuishi maisha mazuri baada ya kumaliza mafunzo ya chuo.
“Tumegundua watoto hususani wa kike wanapomaliza darasa la saba wengine
wanatupwa, wanapata ujauzito na kuepukana mambo kama haya tukaona tuwawezeshe
wapate elimu ya Ufundi, ili waweze kujiendeleza kielimu zaidi,” aliongeza Nitu.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa kituo, Mkurugenzi wa Manispaa ya
Moshi, Rashid Gembe alisema kuwa kituo hicho kitawasaidia watoto viziwi kupata
ujuzi mbalimbali ambao utawawezesha kujiajiri na kuepuka kuwa tegemezi kwa
jamii inayowazunguka.
Nae Mdhibiti wa bora wa Elimu
Manispaa ya Moshi Theresia Mushi,
alisema kuwa uwepo wa chuo hiki utawaongezea thamani na ujasiri watoto viziwi
hasa pale watakapofika mtaani kutokana na ujuzi waliopata kutoka chuoni hapo.