Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amewataka Makarani wa sensa kusimamia kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi ili kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali katika upangaji wa mipango ya maendeleo.
Maagizo hayo aliyatoa wakati akifunga mafunzo ya siku 21 kwa Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya mkoa katika ukumbi wa Chuo kikuu Huria Tawi la Manyara mtaa Korongo mbili.
Alisema kuwa Serikali imedhamiria kujenga uchumi endelevu na kupunguza umaskini kwa wananchi hivyo matokeo ya Sensa hiyo ndio dira ya kupanga mipango ya maendeleo endelevu ya wananchi.
Katika mkoa wa Manyara wamekamilisha ratiba ya Mafunzo hayo na kufanikiwa kupata Idadi wakufunzi zaidi ya 300,ambao watasimamia shughuli ya kuelimisha Makarani kwenye wilaya za mkoa huo.
Nyerere amesema ameridhishwa na matokeo mazuri ya elimu waliopata wakufunzi hasa Matumizi ya zana za kigitali.
Mratibu wa sensa mkoa Gidion Mokiwa amesema ushirikiano miongoni mwa viongozi wa serikali, wawezeshaji na wakufunzi umesaidia kufikia lengo la Mafunzo kwa kuwa wamefanya mifano kadhaa kuhusu elimu hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wakufunzi Mwenyekiti Manase Mndeme ametoa ahadi ya kufanya kazi bora ya sensa kwa Wananchi agosti 23 mwaka huu baada ya Mafunzo ya uhakika.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na NBS ambapo lengo lake lilikuwa kujenga uelewa mpana na wa pamoja kwa wahusika kupata kanuni na mbinu bora za namna ya kukusanya taarifa za kitakwimu nchi nzima kwa kufuata Kanuni za Umoja wa Mataifa.