Na Lucas Raphael,Tabora
MASHINDANO ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na yale ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) Kitaifa yatafanyika mwaka huu Mkoani Tabora.
Akizungumzia mashindano hayo jana Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alisema hiyo ni fursa muhimu sana kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwani itasaidia kuinua vipaji, kutangaza Mkoa na kuwaongezea kipato wananchi.
Alisema maandalizi ya michezo hiyo itakayoshirikisha wanafunzi kutoka Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani yanaendelea vizuri ikiwemo ujenzi wa viwanja mbalimbali vitakavyotumika.
Alibainisha kuwa kinyang’anyiro cha michuano hiyo kinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 29 mwaka huu katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora na ile ya Wasichana ambapo wataanza na michezo ya UMITASHUMTA kisha UMISSETA.
Alitaja baadhi ya michezo itakayoshindaniwa kuwa mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, pete, riadha, mpira wa mikono kwa wavulana na wasichana na mingineyo.
Alibainisha kuwa licha ya ujenzi wa miundombinu ya viwanja hivyo, pia ulinzi na usalama utaimarishwa kuanzia mwanzo wa mashindano hadi mwisho.
‘Tunatarajia kupokea wageni zaidi ya 11,000 kutoka Mikoa mbalimbali wakiwemo wanamichezo, walimu na Maofisa wa serikali, kati yao wanamichezo ni 7,000, walimu 3,000 na Maofisa 1,100 kutoka Tanzania Bara na visiwani,’ alisema.
Mratibu wa Michezo hiyo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kitengo cha Michezo, George Mbijima alisema serikali imetoa kiasi cha sh mil 747 kwa ajili ya ukarabati wa viwanja vyote vitakavyotumika.
Alisema ujenzi wa viwanja hivyo ikiwemo ukarabati wa viwanja vya zamani unaendelea kwa kasi kubwa na vitakuwa tayari kabla ya tarehe ya kuanza mashindano hayo.
Alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kujenga viwanja vya kudumu ambavyo vitaendelea kutumika kwa michezo mbalimbali katika Mkoa husika hata baada ya kumalizika mashindano hayo.
Mwisho
Pichani…Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian ( wa tatu kutoka kushoto) akiwa na Maofisa mbalimbali wenye dhamana ya Michezo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na wale wa Mkoa wakikagua ujenzi wa viwanja mbalimbali katika shule ya sekondari ya Wavulana Tabora na ile ya Wasichana vitakavyotumika kwa ajili ya Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ngazi ya Taifa Mkoani humo kuanzia julai 29 mwaka huu.