Abdullah Thabiti, dereva wa malori bandari ya Dar es Salaam akiiomba serikali iingilie kati kunusuru uchumi wa nchi bandarini
**
MADEREVA wa malori wanaofanya kazi ya kushusha na kupakia makontena kwenye bandari ya Dar es Salaam wamelalamikia utendaji mbovu wa kampuni binafsi ya TICTS iliyokodi eneo la makontena kwa kukosa ufanisi na kusababisha msongamano mkubwa wa malori bandarini, huku madereva wakilazimika kukaa masaa mengi au hata kulala kwenye foleni usiku kucha.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo maarufu kama “Kitopeni” lililo chini ya TICTS ndani ya bandari ya Dar es Salaam, madereva hao, ambao wamekutwa kwenye msongamano wa malori, wameiomba serikali iingilie kati utendaji huo mbovu wa TICTS ili kunusuru uchumi wa nchi.
“Utendaji wa kazi wa TICTS ni mbovu. Sisi madereva kulala nje kutokana na msongamano wa malori na ucheleweshaji wa upakiaji na upakuaji wa makontena unaofanywa na TICTS imekuwa ni jamno la kawaida. Unaweza kulala huku kwenye foleni wiki nzima hujarudi nyumbani na unaambulia kupakua kontena mbili tu au tatu ndani ya wiki nzima,” alisema Zuberi Abdallah Kanjala, mmoja wa madereva aliyekutwa kwenye foleni.
“Gari zinajazana hapa nje ya eneo la makontena bandarini, hatujui zinaingia saa ngapi. Serikali ifuatilie hili tatizo kwa karibu, TICTS ni wapangaji wao, Serikali iwakague utendaji wao wa kazi.”
Naye Abdallah Mkabala, dereva mwingine wa malori aliyeongea na waandishi wa habari kwenye bandari ya Dar es Salaam alisema kuwa ucheleweshaji huo wa kupakia na kupakua makasha au makontena unaofanywa na TICTS huwasababishia madereva wa malori hasara kubwa, kutokana na kulazimika kutumia kipato chao kidogo wanacholipwa kwa siku kununua chakula wakati wanapokesha kwenye foleni mchana na usiku kucha.
“Huwa tunapoteza muda mwingi kwenye foleni hapa eneo la Kitopeni kutokana na ucheleweshaji wa kazi wa TICTS na hii inatuathiri sisi madereva na hata matajiri wetu,” alisema.
Dereva mkongwe wa malori, Abdullah Thabiti, alisema ni aibu kubwa taifa kwa mizigo ya makontena kucheleweshwa kwa muda mrefu bandarini, huku akitaja maeneo ya vifaa na watumishi wa kushusha na kupakia makontena na eneo la kugonga mihuri ya nyaraka za mizigo kuwa ni changamoto kubwa kwenye utendaji kazi wa TICTS.
“HAtuoni raha kukaa hapa tangu saa nne asubuhi hadi sasa saa 10 jioni hatujashusha kontena hata moja. Kontena ziko 600 au 700 sasa utazimaliza kwa siku ngapi kwa spidi hii ndogo?” Thabiti aliongeza.
Ayubu Twalibu, dereva mwingine wa malori ya kontena eneo la bandarini Dar es Salaam, naye amehoji umakini wa TICTS kwenye kazi yake na kulalamikia uzembe kwenye upakuaji na upakiaji wa makontena.
Hivi karibuni umeibuka mjadala mzito kuhusu utendaji kazi wa kampuni binafsi ya TICTS ambayo imekodishwa na serikali eneo la makontena kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20 lakini inalaumiwa kwa kushindwa kuleta ufanisi.
Serikali imethibitisha kuwa iko kwenye mazungumzo kwa sasa na TICTS kujadili iwapo iongezewe mkataba wake kwa miaka mitano zaidi. Hata hivyo, wadau mbalimbali wameibuka na kuitaka serikali kutoiongezea kampuni hiyo mkataba wake.
Chama cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kutoiongezea TICTS mkataba na badala yake irudishe eneo la makontena kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) hadi zabuni ya kimataifa itakapotangazwa ili kuvutia wawekezaji binafsi wa kimkakati wa kuwekeza kwenye eneo hilo la kontena baada ya TICTS kuonekana kushindwa kazi.
ACT-Wazalendo wametaja sababu kama mapato duni, uwekezaji finyu wa TICTS kwenye miundombinu, ucheleweshaji wa mizigo na kushindwa kufikia malengo ya kuongeza idadi ya mizigo ya kontena kama baadhi ya vigezo vinavyofanya TICTS wasistahili kuongezewa mkataba.
Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza hadharani kutoridhishwa na utendaji wa bandari ya Dar es Salaam, ambapo hivi karibuni alimteua Plasduce Mbossa kama Mkurugenzi Mkuu mpya wa TPA ili alete mageuzi kwenye utendaji wa bandari hiyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitishia kuvunja mkataba wa TICTS Aprili mwaka huu kutokana na kampuni hiyo kukosa ufanisi na kuirudisha nchi nyuma katika jitihada zake za kukuza uchumi.