WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro ameagiza Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuhakikisha unasajili kidijitali watoto wote wanaozaliwa mwaka huu hasahasa wale wa mipakani.
Waziri Ndumbaro ametoa maagizo hayo wakati alipotembelea ofisi za wakala huo Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma pamoja na kutembea kituo cha afya cha Namtumbo kujionea zoezi la usajili unaofanywa kwa njia ya kijitali.
“Mkakati wetu namba moja ni kuhakikisha tunaifanya RITA iwe ya kidijitali. Pale katika ngazi ya kijiji, kitongoji kama kuna zahanati basi usajili unaanzia pale kidijitali. Takwimu zinaingizwa na kutumwa Makao Makuu ya Wilaya na baada ya uhakiki na kujiridhisha basi cheti kinatolewa yeye akiwa kule kule kwenye kijiji au kitongoji chake bila kulazimika kusafiri kuja wilayani.
Na tunaanza na Mikoa yote ya mipakani kwa nchi nzima ili kuhakikisha katika mwaka huu wa fedha kila mtoto atakayezaliwa anasajiliwa,” amesema Waziri Ndumbaro.
Amewataka pia Maafisa Elimu wa Shule za Msingi na Sekondari kuhakikisha watoto wote watakaoandikishwa wawe na vyeti vya kuzaliwa na kusisitiza kuwa mkakati huo ukitekelezwa vyema kwa ushirikiano mpaka kufika mwaka 2025 kutakuwa hamna mtoto ambaye atakuwa hana cheti.
Ameongeza kuwa maelekezo hayo ni ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anataka mpaka atakapomaliza kipindi chake cha uongozi, Watanzania wote wawe na vyeti vya kuzaliwa na kusema kuwa wizara yake itahakikisha hilo linafanikiwa katika kipindi kilichopangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Dk Julius Ningu amesema kuwa watahakikisha wanatoa elimu zaidi kwa wananchi ili waweze kujua umuhimu wa kuhakikisha watoto wanakuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Naye Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa amepongeza utaratibu huo wa kusajili na kutoa vyeti kidijitali kwani utawarahishia wananchi wengi waliokuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa, kifo au talaka na kusema hatua hiyo itaongeza usajili zaidi.
Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa RITA Bi. Angela Anatory ametoa wito kwa wanajamii kuchukua vyeti vya kuzaliwa au vya vifo mapema badala ya kusubiri matukio kama ya usaili na kujiunga na elimu ya juu ndo waanze kukimbizana kutafuta vyeti hivyo na kuongeza kuwa ofisi yake itaendelea kutoa elimu zaidi hasa kwa wananchi wa vijijini.