Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo akizungumzia huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT ambayo inafanyika kwa kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida limeanzisha utaratibu
wa kusikiliza mahitaji na kupokea ushauri wa wananchi na kupokea maoni yao kuhusu
sekta ya nishati ya umeme katika wilaya zote ili ziweze kufanyiwa kazi kwa
kuwafuata katika maeneo yao.
Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege
akizungumza leo Julai 26, 2022 na Wananchi wa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama
wakati akisikiliza mahitaji na ushauri wao kuhusu sekta ya nishati ya umeme alisema
utaratibu huo ambao kwa mara ya kwanza umeanza kufanywa katika kata hiyo akiwa
na mwezi mmoja na wiki mbili tu tangu afike mkoani hapa akitokea mkoani Ruvuma kuwa
utakuwa endelevu.
“Utaratbu huu utafanyika katika kata na wilaya zote mkoani hapa na ninyi
wana Iguguno mmekuwa wakwanza kusikilizwa hivyo tumekuja kuwasikiliza ili tutatue
changamoto zenu na kupokea ushauri na maoni yenu tuweze kuboresha huduma za shirika letu ziwe
nzuri na kila mwananchi aweze kunufaika nazo” alisema Mwakasege.
Alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kuwasikiliza na kupokea ushauri wao
na kama kutakuwa na maeneo yenye ukakasi waweze kuyachukua na kuyafanyia kazi ili
kila mmoja aweze kutumia huduma hiyo kwa usalama ambayo licha ya kuwa nzuri lakini ikitumika vibaya ni inakuwa ni hatari.
Alisema wao kama wasimamizi wasipowaeleza madhara hayo itakuwa vigumu
kuyajua ndio maana wameanzisha utaratibu huo wa kukutana nao ili kufahamishana
mambo mbalimbali na kupokea maoni waliyonayo.
Mwakasege alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa kata hiyo kwa
kuratibu mkutano huo pamoja na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi na kueleza
mahitaji yao mbalimbali.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika katika viwanja vya ofisi ya mtendaji wa
kata hiyo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kutoka kwa wananchi ni kuomba
kupelekewa umeme katika maeneo ambayo hayana huduma hiyo , kupunguziwa gharama
za kufungiwa umeme kutoka Sh.27,000 hadi zaidi ya Sh.300,000 ambayo wengi wao
hawezi kuimudu .
Katika hatua nyingine wananchi hao walilipongeza shirika hilo Mkoa wa
Singida kwa kuanzisha utaratibu wa kwenda kusikiliza mahitaji na ushauri wao na
kwa kipekee wakimpongeza Meneja Mwakasege kwa kuanzisha utaratibu huo na kueleza
shirika hilo jimejipanga kufanya kazi kwa spidi anayoitaka Rais Samia Suluhu
Hassan ya kufanya kazi kwa bidii ili kuwatumikia wananchi.
Wananchi hao walimuambia Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi
Mwakasege kuwa kutokana na mji wao kuwa mkubwa wapo tayari kutoa eneo la
kujenga ofisi ya Tanesco ili waachane na kupanga na wanachotakiwa kukifanya ni
kuandika barua ya maombi ya kuomba eneo hilo na kuipeleka ofisi ya kijiji.
Aidha katika mkutano huo Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco
Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo alielezea huduma mpya ya maombi ya
kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT ambayo inafanyika kwa
kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za
shirika hilo.
Katika mkutano huo Meneja huyo aliongozana na Meneja wa shirika hilo Wilaya
ya Mkalama, Mhandisi Benedict Ryeimamu, na Fundi Umeme wa Kituo cha Tanesco,
Kata ya Iguguno, Kasimu na Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa
wa Singida, Rehema Mwaipopo.