*************************
Na Joseph Lyimo
WILAYA ya Simanjiro Mkoani Manyara imeongoza kwa asilimia 119 kwa wananchi wa Mkoa huo kupata chanjo ya UVIKO-19 kwenye wakati huu ambapo zoezi la wananchi kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya UVIKO-19 ikiendelea maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchanjaji UVIKO-19 yaliyotolewa hivi karibuni kwenye Halmashauri saba za Wilaya za Mkoa wa Manyara, Halmashauri ya Simanjiro imeongoza kwa kupata asilimia 119.
Halmashauri ya Wilaya ya Babati, imeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 78, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imeshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 69 na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, imeshika nafasi ya nne kwa kupata asilimia 67.
Halmashauri ya Mji wa Babati imeshika nafasi ya tano kwa kupata asilimia 58, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeshika nafasi ya sita kwa kupata asilimia 56 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeshika nafasi ya saba kwa wananchi wake kuchanja UVIKO-19 kwa asilimia 54.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mbaraka Alhaji Batenga amewapongeza viongozi, wataalamu wa afya na wananchi wa Simanjiro ujumla kwa kuhamasika na kufanikiwa kuongoza kiwilaya kwenye kushirikia kupata chanjo ya UVIKO-19.
“DMO (Mganga mkuu wa Wilaya), wataalamu wa afya na jamii kwa ujumla, ninawapongeza kwa namna mnavyoshughulikia suala hili la kitaifa kwani inaonyesha ni namna gani mnajitoa katika kutoa elimu kwa watu katika kuhakikisha wanashiriki kwa hiyari kupata chanjo,” amesema Batenga.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kiteto ambaye anakaimu Wilaya ya Simanjiro, amesema anatarajia wananchi ambao hawajapata chanjo ya UVIKO-19 watashiriki kupata chanjo hiyo ambayo inaendelea kutolewa na wataalamu wa afya.
“Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakituasa wananchi kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani maradhi hayo bado yapo nchini hivyo tushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19,” amesema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga Laizer amewashukuru wananchi kwa ujumla na wataalamu wa afya kwa namna walivyotekeleza shughuli hiyo ya zoezi la chanjo ya UVIKO-19.
Amesema mwitikio wa viongozi na wananchi katika kupokea suala la chanjo ya UVIKO-19 imesababisha shughuli hiyo iende kama ilivyopaswa na matokeo chanja yakaonekana kwa Simanjiro kuongoza.
“Niwaombe viongozi wa dini, wazee wa kimila, viongozi wa kisiasa na serikali na wananchi kwa ujumla, tushiriki kupata chanjao na yule ambaye bado hajapata chanjo ya UVIKO-19 apate ili ajilinde na maradhi hayo,” anasema Mwenyekiti huyo wa Halmashauri hiyo.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro (DMO) Dkt Aristidy Raphael amesema halmashauri hiyo imeongoza kwenye uchanjaji mkoani humo kutokana na mwitikio mkubwa wa jamii uliopo hivi sasa.
“Tunawapongeza wananchi wa Simanjiro kwa kuitikia hili na kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani baada ya kupata elimu na kutambua umuhimu wa chanjo waliridhia na kukubali kupata chanjo hiyo,” amesema Dkt Raphael.
Ametoa wito kwa wananchi wa Simanjiro ambao bado hawajashiriki kupata chanjo ya UVIKO-19, wahakikishe wanapata kwani Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa matangazo mbalimbali kwa wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19.
Amesema wataalamu wa afya wanatembelea makundi mbalimbali ya wananchi wa Simanjiro kuanzia wafugaji, wakulima, wachimba madini, wavuvi, wafanyabiashara na watu wa kada mbalimbali ili wawafikie na kuwahudumia.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Simanjiro, wanaeleza kuwa wamehamasika kupata chanjo hiyo ya UVIKO-19 ili kujikinga na gonjwa hilo kwani wataalamu wa afya wamewapa elimu ya kutosha.
Mkazi wa kitongoji cha Manyara, Elijah Ngao amesema hatua ya wananchi wa Wilaya Simanjiro kujitokeza kuchanja kwa wingi chanjo ya UVIKO-19 inatokana na hamasa iliyotolewa na wananchi kupatiwa elimu kuwa chanjo hiyo haina madhara.
“Mara nyingi kitu kigeni kikitokea kuna baadhi ya watu wanapotosha na kuzungumza ndivyo sivyo juu ya jambo hilo utadhani wanalitambua kumbe hawafahamu ila hili la UVIKO-19 wengi wao wamelitambua na kulielewa ndiyo sababu wamejitokeza kwa wingi kuchanja,” anasema Ngao.
Amesema baada ya maneno ya uongo na dhana potofu kuonekana kuwa ni propaganda zisizo na maana yoyote, wananchi wameamua kushiriki chanjo ya UVIKO-19 kwa manufaa yao.
“Mtu anaona atapata maambukizi ya UVIKO-19 yeye mwenyewe na hayo ni maradhi ambayo hayana matibabu hivyo ameona hawezi kupata tatizo kisa kutochanjwa kwa kutosikiliza wataalamu wa afya na kuwasilikiza wazushaji,” anaeleza.
Mkazi wa kata ya Shambarai John Issangya anasema wataalamu wa afya wamekuwa wanafika hadi vijijini na kutoa elimu kwa jamii kIsha kuwapatia chanjo hiyo ya UVIKO-19.
“Hadi hivi sasa elimu inaendelea kutolewa kwa jamii huku vijijini na wanaitikia ushauri wa kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 kwani wanatambua kuwa ukipata maradhi hayo bila kuchanja utapata matatizo makubwa kwenye changamoto ya kupumua pindi ukiupata ugonjwa huo,” anasema.
Mkazi wa kata ya Endiamtu Mashaka Jororo anasema kuwa viongozi na wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kwa pamoja wameungana katika kuhakikisha wanapata chanjo ya UVIKO-19 ndiyo sababu wakaongoza kushika nafasi ya kwanza.
“Siyo jambo dogo Simanjiro kushika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri saba za Wilaya kwa hapa Manyara, binafsi niwapongeze wana Simanjiro kwa kufanikisha hili na kuongoza,” anasema Jororo.
Anasema anatarajia wananchi wa wilaya ya Simanjiro wataendelea kupata chanjo ya kujikinga na janga la UVIKO-19 kwa kuwasikiliza viongozi wa Serikali na wataalamu wa afya na siyo vinginevyo.
Hivi karibuni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza hivi karibuni kwenye tamasha la MZIKI MNENE lililofanyika uwanja wa Nangwanda Mkoani Mtwara amesema imethibitika kuwa njia ambayo ni salama ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 ni kupata chanjo kwani ukichanja utakuwa umejikinga na kuikinga jamii ya watanzania.
Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea kuwalinda wananchi wake katika maambuzi ya magonjwa mbalimbali kwa kutoa chanjo ikiwemo ya UVIKO-19.
“Sisi kama Wizara ya Afya tutatumia mbinu mbalimbali ambazo zitakazowafikia wananchi kama tunavyotumia matamasha haya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupata huduma ya chanjo ya UVIKO-19,” anamaliza kwa kusema Waziri Ummy.