Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma ameomba mfuko wa Mama Rais Samia Suluhu Hassan, uwafikie ipasavyo ili kufanikisha ujenzi wa barabaza zitakazosafirisha wananchi na mazao kwa lengo la kuwanyanyua kiuchumi.
Hhayuma akizungumza mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kupitia mfuko wa Mama, wataweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia miundombinu ya barabara.
Amesema anashukuru kwa kupata shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwenye mji mdogo wa Katesh na kuongezewa shilingi milioni 280 kwa ajili ya usanifu wa kina.
Amesema kutoka Wilaya ya Hanang’ hadi Kondoa ni kilomita 70 ila kutokana na ubovu wa miundombinu inachukua muda mrefu kufika hivyo barabara ya lami kutoka Kibrash mkoani Tanga inayopitia Kondoa iunganishwe na Hanang’ ili kuondoa changamoto hiyo.
“Barabara ya kutoka Nangwa kupitia Gissambalang’ kisha Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma, ikijengwa kwa kiwango cha lami itarahisisha usafirishaji,” amesema mhandisi Hhayuma.
Amesema barabara hiyo ikiunganishwa kwa lami itafungua fursa ya maendeleo kwa wananchi wa wilaya ya Hanang’ kwani makao makuu ya nchi Dodoma patakuwa ni karibu.
Amesema kupitia mfuko wa Mama anatarajia barabara za eneo hilo ikiwemo ya Mogitu-Haydom zitajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi kunufaika nazo.