Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael leo Julai 27, 2022 jijini Dar es Salaam amefungua kikao kazi cha Maandalizi ya Mpango kazi wa utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya elimumsingi ikiwemo ufundishaji wa Kiswahili nchini Afrika Kusini.
Akifungua kikao hicho Katibu Mkuu Michael amesema utekelezaji wa Hati hiyo pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu msingi nchini utaimarisha ushirikiano wa muda mrefu ambao Tanzania na Afrika Kusini wamekuwa nao.
Katibu Mkuu huyo amesema amefurahishwa kuona utekelezaji wa Hati hiyo umeanza mapema kwa kuwa ndio ilikuwa nia ya viongozi wa nchi kuona utekelezaji wake unaanza mara moja ili pamoja na mambo mengine kiswahili kianze kufundishwa nchini Afrika Kusini.
“Utiaji saini wa Hati ya Makubalino ya ushirikano kwenye elimumsingi uliofanyika mapema mwezi Julai, 2022 ulishuhudiwa na Mhe. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na alisisitiza kutocheleweshwa kwa utekelezaji wake hasa ufundishaji wa Kiswahili nchini Afrika ya Kusini na leo mmeanza kazi nimefurahi sana,” amesema Katibu Mkuu Michael