MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza wakati wa kikao hicho kushoto ni Kamisa wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Anna Makinda na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Pili Manyema akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa
Na Oscar Assenga, TANGA.
ZAIDI ya watanzania Milioni 61 wanakadiriwa kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakalofanyika Agosti 23 mwaka huu hapa nchini.
Hayo yalisemwa na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda wakati wa kikao cha viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Tanga,Serikali wakiwemo wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri.
Alisema Sensa ni kitu muhimu kinachoipa Serikali ubora wa kufanya kazi zake na ya mwaka huu itakuwa tofauti kabisa ndio maana wakadiria watanzania milioni 61 hadi 64 kutokana na uzazi walioupata mwaka 2012 walikuwa wakiongeza kwa asilimia 2.9.
Alisema suala la Sensa ni takwa la kisheria na ni ustarabu wa kuendesha serikali mbalimbali ulimwenguni kutokana na kwamba unapokuwa na watu basi uwajue ili uweze kupanga mipango yako vizuri.
“Lengo la Sensa ni kujua idadi ya watanzania kama ham hesabiani itakuwa ni fujo sana kuweza kuendesha nchi hivyo ni jambo muhimu kama kiongozi lazima ujue idadi ya watu wako”Alisema
Alisema kwamba sensa ya mwaka huu itakwenda kidigitali na mpaka sasa sasa makarani waliotenga maeneo wanayo kabisa kwamba kitongoji hiki kina nyumba ngapi na hali gani na kitu gani.
Aidha alisema kutokana na hilo hakuna namna karani wa Sensa anaweza kuruka nyuma ataonekana toka Dodoma na wamechukua picha za Satelite kila nyuma inaonekana kwa maana wanahesabu na majengo pia.
Kamisaa huyo alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana kuwasiliana na watu kwa karibu sana hivyo ni muhimu wakatumia nafasi zao kuhamasisha zoezi hilo kwenye madhehebu yao.
“Viongozi wa dini ni mwakilishi wa Mungu ,watu wanawasikilizeni mkisema hawafanyi ubishi na viongozi wa mila pia watu wana watii sana hata waganga wa kienyeji wanaheshimika kama mtu anaweza kulala huko kugaragara hao watu wanaaminika kwa asilimia kubwa”Alisema Kamisaa.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alisema watu ambao watataka kuhujumu zoezi la Sensa watatumia sheria kali dhidi yao kwa sababu watakuwa hawana nia ya maendeleo.
Alisema suala la sensa ya watu na makazi ni jambo muhimu sana hasa kwenye kupanga maendeleo ya nchi na mgao wa rasilimali kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya na ujenzi wa miundombinu na nyengine zote.
Malima alisema huko nyuma zoezi hilo lilikuwa likipata shida kidogo kutokana na kutokufahamu kwamba viongozi wa dini wanasikilizwa sana kwenye maeneo yao hivyo hakikisheni mnalihamasiha.
Alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika madhehebu yao kulihamasisha suala hilo ili kuhakikisha waumini wao wanashiriki kwenye zoezi hilo la kuhesabiwa kutokana na kwamba kila mtu anamuamini kiongozi wa kiroho.