Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza akizungumzia kuhusu ofisi ya Ardhi Mkoa wa Singida ilivyoanza leo Julai 25,2022 kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wananchi kwa kila halmashauri ili ziweze kutatuliwa.
Na Dotto Mwaibale, Singida
OFISI ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Singida imeanzisha utaratibu wa
kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wananchi kwa kila halmashauri ili
ziweze kutatuliwa.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, akizungumza leo
Julai 25, 2022 alisema utaratibu huo ambao utakuwa endelevu unalenga kupunguza
au kumaliza kero za migogoro ya ardhi ambayo baadhi zimekaa muda mrefu bila
kutatuliwa..
Hoza alisema maofisa ardhi wa halmashauri zote wahakikishe wanatenga muda
wao wa kushughulikia kero za ardhi katika siku maalum zilizopangwa na
kuzitatua.
Alisema hakuna sababu kwa wananchi kusubiri hadi ziara za viongozi wakuu
ndipo watoe malalamiko yao ya kero ya migogoro ya ardhi hivyo watumie muda wao
kupeleka migogoro yao kwa maafisa ardhi ili iweze kutatuliwa.
Katika siku ya kwanza ya zoezi la kusikiliza kero za migogoro ya ardhi watu
wengi wamejitokeza katika ofisi ya zamani ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Singida vijijini kwa ajili ya kupeleka kero zao kwa maafisa ardhi.
Baadhi ya wananchi waliofika kutoa kero zao za migogoro ya ardhi
iliyotofautiana akiwepo Maulid Ndui,
Abdillah Said kutoka Puma wilayani Ikungi, Khalifa Matali kutoka
Manispaa ya Singida, Mathew Mpaji kutoka Dung’unyi wilaya ya Ikungi na Zuhura
Salum kutoka maeneo ya Sabasaba Manispaa ya Singida walimshukuru Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuhimiza watendaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kuacha kukaa ofisini badala yake watoke kwenda kusikiliza kero
mbalimbali zinazotokana na migogoro ya ardhi nchi nzima.
Aidha wananchi hao walimpongeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida,
Shamim Hoza na watendaji wa ofisi hiyo kwa kutekeleza agizo la Serikali kwa
kuanza kuwasikiliza wananchi wenye kero za migogoro ya ardhi ili ziweze
kutatuliwa haraka iwezekanavyo.
Wananchi hao walisema hatua hiyo imewapunguzia adha ya kusafiri kwenda Dar
es Salaam na Dodoma kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao ambapo hapo awali
walikuwa wakipote muda na fedha wakati wa kushughulikia mogogoro hiyo.
“Kwa kweli niipongeze wizara hiyo na Kamishna Hoza kwani hii walioichukua
itasaidia kuwafanya watu wengi wenye migogoro ya ardhi ambao walikuwa hawana
uwezo kuja kwa wingi kuleta kero zao” alisema Zuhura Salum.
Aidha Zuhura Salum aliiomba ofisi ya ardhi Mkoa wa Singida kuongeza siku za
kusikiliza migogoro hiyo kutoka siku moja na kuwa wiki moja kutokana na wingi
wa wananchi wenye malalamiko mbalimbali yanayohusu ardhi.