**********************
Jeshi la Polisi Nchini limetoa onyo kwa baadhi ya madereva wa magari makubwa ya mazigo (malori) wanaohamasisha mgomo wa madereva ili kuzuia magari mengine yasifanye shughuli za usafirishaji kwa kisingizio cha madai ya haki zao wanazodai kutoka kwa waajiri wao kutokuwalipa posho zao na kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Kamishna wa Operesheni na Mafunzo CP Awadhi Juma Haji, amesema kuwa, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa wanaotumia kisingizio cha mgomo huo kuzuia madereva wengine wasitoe huduma za usafirishaji na kuwataka wafuate taratibu za kisheria.
Aidha, kamishna Awadhi amewaagiza Makamanda wa Polisi wa mikoa kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaobainika kuhamasisha madereva wenzao kufanya mgomo huo.