Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa jitihada zake katika kuhifadhi rasilimali za wanyamapori na kuongeza pato la Taifa.
Waziri Chana alitoa pongezi hizo jana tarehe 23 Julai, 2022 alipotembelea Mapori ya Akiba ya Ikorongo Na Grumet yanayopatikana katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Akizungumza, wakati wa ziara hiyo Waziri Chana aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ipo bega kwa bega na Taasisi zote za uhifadhi na aliwataka Menejimenti ya Taasisi hizo ikiwemo TAWA kuwasilisha mahitaji na changamoto zote zinazohitaji Wizara na Serikali kwa ujumla kuzitatua.
Aidha, katika ziara hiyo Waziri Chana alipata wasaa wa kuzungumza na wawekezaji kutoka kampuni ya Grumeti Reserve.
Naye, Kamishna Msaidizi – Uhifadhi wa Kanda ya Ziwa Julius Wandongo, alimshukuru Waziri Chana kwa kutembelea Mapori ya Akiba Ikorongo na Grumet na aliahidi kutekelezwa kwa maelekezo yaliyotolewa.