*********************
Adeladius Makwega-DODOMA
Wakristo wametakiwa kujikabidhi kwa Mwenyezi Mungu na kuwa tayari kutambua kuwa binadamu ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu na mambo yote ya maisha yao yatakwenda salama na sawia. Hayo yamesemwa na Padri Paul Mapalala Paroko wa Kanisa la Bikira Maria Immakula parokia ya Chamwino Ikulu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma
“Sisi binadamu mara nyingi tunakwenda kinyume na mpango wa Mwenyezi Mungu, lakini pale tunapokwenda kinyume bado Kristo ametuachia Sakramenti nyingi, tuwe kweli watoto wa Mungu, tutumie Sakramenti ya Upatanisho inayotukumbusha kila tunapoanguka tumkimbilie huyo huyo Mwenyeenzi Mungu, ili aweze kutusamehe makosa yetu na tusimame imara tukitembea katika miguu iliyo salama.”
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki parokiani hapo aliongeza kuwa vishawishi lazima vitakuwepo lakini binadamu anapaswa kukabiliana navyo. Kila mkristo anatakiwa kusali sala ya baba yetu, hapo wataeleza mengi yaliyo ndani ya mioyo yao kwa Mungu kwani Mungu ndiye aliyemuumba binadamu.
“Ulituonesha Baba yetu wa Mbinguni, utusaidie kumpenda Mungu, kama Baba yetu ambaye anatutunza kwa wema wake.”
Hilo lilikuwa ni miongoni mwa maombi kadhaa ya misa hii ya jumapili ya 17 ya mwaka C wa Kanisa Katoliki.
Mwandishi wa ripoti hii ameshuhudia hali ya hewa ya eneo la Chamwino Ikulu ikiwa ya baridi kali kwa vipindi vya asubuhi, jioni na usiku huku mchana kukiwa na jua linalowaka kwa kadili na kwa mbali kukiwa na upepo unavuma kiasi.