Na Mathias Canal, Rombo
Hivi karibuni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Isidor Mpango wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Rombo alitangaza serikali kuanza ujenzi wa Kilomita 5.5 za barabara ya lami.
Alitoa maagizo kwa wizara ya ujenzi inayoongozwa na Waziri wa Ujenzi Mhe Prof Makame Mnyaa Mbarawa kuhakikisha kuwa inaanza haraka iwezekanavyo ujenzi wa barabara hiyo inayoanzia eneo la Mlembea mpaka kijiji cha Uwanda.
Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku saba katika Jimbo la Rombo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na Kata ya Holele Mbunge wa jimbo hilo ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amewaeleza wananchi dhamira serikali ya ujenzi wa barabara hiyo.
Amesema kuwa barabara hiyo itarahisha utoaji huduma za afya kwa wagonjwa wanaoenda kupatiwa matibabu.
Kadhalika amesema kuwa barabara hiyo itarahisisha utoaji huduma za usafirishaji wa mazao ya chakula na ufanyaji wa biashara kwa wananchi wa jimbo la Rombo pamoja na wale wa wilaya na mikoa ya jirani.
Kuhusu biashara, Prof Mkenda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kufungua mipaka na wananchi wameweza kuuza bidhaa mbalimbali nje ya nchi ikiwemo biashara ya mazao.
Prof Mkenda amesisitiza kuwa wananchi wa Rombo watasimama na Rais Samia kwa kumuunga mkono kutokana na ufanisi mkubwa anaouonyesha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini.