Na. WAF – Mtwara
Imethibitika kuwa njia ambayo ni salama ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 ni kupata chanjo hiyo kwa kuwa ukichanja utakuwa umejikinga na kuikinga jamii ya watanzania.
Hayo ameyasema Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Julai 23, 2022 kwenye tamasha la MZIKI MNENE lililofanyika katika kiwanja cha Nangwanda mkoani Mtwara.
Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea kuwalinda wananchi wake katika maambuzi ya Magonjwa mbalimbali kwa kutoa chanjo ikiwemo ya UVIKO-19.
“Sisi kama wizara ya Afya tutatumia mbinu mbalimbali ambazo zitakazowafikia wananchi kama tunavyotumia matamasha haya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupata huduma ya chanjo ya UVIKO-19. ” amesema Waziri Ummy
“Tumefurahi kuona wananchi wengi wa Mtwara wamejitokeza katika kupata huduma hii ya chanjo na tunaamini mikoa mengine watajitokeza kama walivyojitokeza mkoa huu.
Aidha, Waziri Ummy ametoa shukrani kwa Serikali ya Marekani (USAID) kwa kutoa fedha za kuwahamasisha wananchi kuchanja na kuahidi kuendelea kutumia fedha hizo katika njia nyingine zitakazo saidia wananchi kujitokeza kuchanja kama njia hii ya MZIKI MNENE.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Gen. Marco Gaguti amesema zoezi hili nitaendelea katika maeneo mengine mkoani hapa kwa kuwa wanamtwara wameelimika na wameamua kuchanja kwa kujua umuhimu wa chanjo.
“Tamasha hili la MZIKI MNENE limesaidia sana kuwahamashisha wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuchanja hivyo tunawashukuru kwa kujitokeza kuchanja kwa wingi.” amesema Brig. Gen. Gaguti