Adeladius Makwega-DODOMA
Msomaji wangu leo hii nataka kulieleza jambo moja muhimu sana ili kila mmoja wetu afahamu, nitajaribu kulieleza jambo hili kwa majaliwa ya Mungu na kwa lugha ya kawaida sana, hili jambo hili lieleweke kwa namna niliyokusudia.
Kuna rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia neno Halmashauri linatokana na neno la kiarabu Al-Mashaur likimaanisha mambo mengi mengi. (mashauri mashauri), sifahamu ukweli wa maelezo hayo lakini nimewahi kusimuliwa hilo.
Ni ukweli uliowazi kuwa halmashauri ina mambo mengi sana, leo nimekusudia kulieleza jambo moja tu nalo ni hili,
Katika kila Halmashauri za wilaya nchini Tanzania huwa na vikao saba vya Baraza la Madiwani (BLM) ambapo vikao vinne ni vya robo ya mwaka, robo moja ikiwa na miezi mitatu.Lakini kuna vikao vingine vitatu, navyo ni kikao cha bajeti, kikao cha hesabu za mwisho na kikao cha hoja(KH).Hiki ni kikao pekee ambacho mwenyekiti huwa ni mkuu wa mkoa ilipo halmashauri husika.
Katika hoja zinazopelekwa mbele ya vikao vya madiwani ni hoja tatu ya kwanza hoja za mkaguzi wa nje, ya pili ni hoja za mkaguzi wa ndani na hata hoja za ukaguzi maalumu pia inapokelewa na kujadiliwa.
Hoja za mkaguzi wa nje baada ya kusomwa bungeni kile kitabu chenye hoja hizo panatazamwa ukurasa wa Halmashauri husika. Hoja hizo zinasomwa na zinajibiwa moja baada ya nyingine, mkishajibu, majibu yote na viambatanisho vyake yanapelekwa kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG). Yeye (CAG) atapitia hoja zote, majibu na viambatanisho kama ataridhika nayo anaweza kuzifuta na zile ambazo ataamua vinginevyo zinabaki. Hapo mwanakwetu ndipo yanaibuka maneno yale mbona hoja hii ina miaka miwili mbona hoja hii ina miaka mitatu haijafutwa/ hatua gani zimechukuliwa?
Baada ya hapo ndipo vitaanza vikao vya halmashauri tangu Kikao cha Wataalamu (CMT), hoja hizi zikitoka hapo zinapitia Kamati ya Ukaguzi ambayo kunakuwa na wajumbe watano kutoka taasisi za serikali jirani na Halmashauri hiyo. Wao watapitia hoja zote nakutoa maoni yao. Zikitoka hapo zinakwenda Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya wilaya hiyo ambapo kunakuwepomwenyekiti, Katibu (mkurugenzi Mtendaji) na wajumbe(madiwani) na wakuu wa idara kadhaa watatoa maoni yao. Hapa pia akiwamo Katibu Tawala wa Wilaya(DAS) akiingia kwa upande wa wataalamu kama Wilaya yake ina Halmashauri mbili basi kote huko anawajibu wa kushiriki. Maoni yatatolewa na mwisho hoja hizo zitapelekwa katika kikao cha madiwani cha hoja chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa(RC)
Kwa Hoja za Mkaguzi wa Ndani hizi kama hazijafutwa basi zinaigizwa katika hoja za mkaguzi wa nje, kwa kuwa mkaguzi wa nje anaweza kuzipitia hoja za mkaguzi huyu (ndani) na kama hazikufutwa yaani majibu hayakupatikana na kama yalipatikana hakulidhika nayo
Ifihamike wazi kuwa hoja za mkaguzi wa ndani zenyewe zinapitia hatua zile zile za hoja za mkaguzi wa nje lakini hoja hizo zitaingia katika BLM la vikao vile vya robo kwa maazimio yake tu chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri(siyo RC)
Naomba msomaji wangu nirudie hili, fahamu kuwa katika vikao vyote vya wataalamu vya halmashauri ya wilaya-Ofisi ya Mkuu wa Wilaya anashiriki DAS kama mjumbe wa wataalamu vikao vyote. Ndiyo kusema kama mchango wake wa mawazo ambao ni vigumu kutafautiana na Mkuu wa Wilaya (DC) utakuwa unatolewa katika kila kikao anachoshiriki DAS kama mjumbe halali.
Katika kila kila kikao cha Baraza La Madiwani mkuu wa wilaya na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama wanaingia na kuufuatilia mjadala wote mwanzo mwisho isipokuwa kama baraza litageuka kuwa kamati lakini huko pia DAS atakuwepo kama mtaalamu na wakuu wa Idara wengine.
Ndiyo kusema katika wilaya yoyote nchini Tanzania kwa miongozo ya uendeshaji wa Serikali za Mitaa (SM) ni vigumu mno DAS na DC kutokulifahamu jambo lolote. Isitoshe hata wakihitaji nyaraka za aina yoyote ile (hata za siri) wakiomba kwa barua wanapatiwa kwa kuwa DC ndiye mwakilishi wa rais wilayani na eye ndiye muulizwa wa kwanza kutoka kwa viongozi wakuu kama Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na hata Rais.
Msomaji wangu fahamu kuwa katika kila BLM, Katibu Tawala Mkoa(RAS) anawajibika kushiriki vikao vyote saba nilivyovitaja, kiti chake kinakuwepo katika kila kikao. Lakini cha kusikitisha maRAS wengi wanatuma uwakilishi tu isipokuwa kwa kikao kimoja kile cha Hoja za Ukaguzi.
“Kazimbaya jitahidi muwasiliane na wakurugenzi wenzenu, mpange tarehe tafauti ili niweze kushiriki vikao vyote vya Mabaraza ya Madiwani.” Haya aliyasema sana Mhandisi Zena Said akiwa RAS wa Tanga wakati huo ambaye sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (SMZ). Dada yangu huyu alijaliwa hilo, sifahamu MARAS wengine kama wamejaliwa hilo.
Nachotaka kusema kwa jumla hakuna hoja yoyote ya Halmashauari ambayo kwa ukweli wa Mungu haifahamika kwa DAS, DC, RAS na RC. Hivyo ndivyo nchi yetu tangu enzi ilivyopanga uendeshaji wa Halmashauri zetu chini ya Serikali za Mitaa(SM) na Serikali Kuu (SK) ambaye ndiye msimamizi.
Kama kuna DAS, DC, RAS na RC hawalifahamu jambo basi hiyo ni shida ya mtu binafsi kwa kutokutimiza wajibu wake.
Katibu Mkuu TAMISEMI anapelekewa nakala zote za vikao vyote vya Halmashauri nchi nzima, Swali ni je nakala hizo zinasomwa au zinapelekwa National Archieves? Anawajibu wa kuzisoma neno kwa neno ili atoe ushauri sahihi, maelekezo sahihi na maamuzi sahihi kwa taifa letu.
Sasa inawezekana kukawa na hoja za ukaguzi maalumu ambao umeagizwa na viongozi wakuu wa serikali kimkoa au kitaifa. Pia ukaguzi maalumu unaweza kuagizwa na CAG mwenyewe na hata TAKUKURU ili waweze kulifahamu kwa kina jambo fulani wanalolichunguza.
Kuhitimisha matini yangu kwa leo ni wajibu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo tangu wananchi, watumishi wa kawaida hadi viongozi wa ngazi zote serikalini.
Kama limefanyika zuri ni la serikali na kama jambo limeharibika nalo ni la serikali. Maana serikali ni ya wote wananchi na viongozi wao wa ngazi zote.
Viongozi wa kitaifa wajitahidi mno wanapofika katika kila wilaya wakumbuke kuwatia moyo wananchi hilo linawafanya wananchi wawapende viongozi wao wa ngazi zote. Lawama zisiwekwe hadharani, unaweza kudhani kosa ni la Mkurugenzi Mtendaji kumbe mwenye kosa ni DAS, DC, RAS au RC.
Hilo kosa ambalo unadhani wamefanya hao, kwa wananchi wa kawaida wanaingiza serikali nzima ndani yake na chama kinachotawala. Tujitahidi sana, viongozi wa ngazi zote wazungumze na kuelezana ukweli bila unafiki katika vikao vya ndani. Wakitoka nje wote wanakuwa kitu kimoja kwa kuwa jahazi linaelea na wote na likizama na wote.
Viongozi wote wanapaswa kuelezana ukweli wakiwa vikaoni ndani narudia tena mwanakwetu, natambua wanaweza kuibuka wale wanaokasirika, mabingwa wa kukasirika wafahamu kuwa serikali ni mali wa watu si ya mtu mmoja, viongozi wote kila mmoja ngazi zote wafahamu wapo hapo kwa niaba ya umma.(siyo mtu mmoja)
Kwa maana serikali ya mtu mmoja aliondoka nayo Edward Twining mwaka 1961(Tanganyika) na Rafiki yake Sultan Jamshid Bin Abdulla mwaka1964 (Zanzibar).
Hata ukiondoka katika uongozi huko ulipo tutakufuata, ukiwa mvuvi tutakwambia vua samaki wakubwa hawa wadogo waache wakue, ukilima lima kilimo bora kwa kufuata kanuni bora za kilimo usije ukakosa chakula ukafa na njaa, ukijenga nyumba weka choo ili usilete kipindupindu kwa wenzako watu wakafa. Mwanakwetu serikali ya watu hakuna kununa wala kukasirika.