MRADI wa maji wa Bwawa la Nsenkwa unaotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Mlele Mkoani Katavi unatarajia kunufaisha wakazi zaidi ya 68,000 wanaoishi katika Vijiji 16.
Mradi huo uliopo katika Kijiji cha Nsenkwa, Kata ya Nsenkwa Wilayani humo unaotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maji hadi kukamilika kwake unatarajia kugharimu kiasi cha sh bil 2.9.
Akizungumza na gazeti hili Meneja wa RUWASA Wilayani hapa Mhandisi Gilbert Isaac alisema bwawa hilo ni chanzo muhimu sana cha maji kitakacho punguza adha ya upatikanaji huduma ya maji safi kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Alisema wakazi 68,426 wanaoishi katika jumla ya vijiji 16 vya halmashauri ya wilaya hiyo wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji ambayo hayatoshelezi mahitaji yao.
Mhandisi Isaac alibainisha kuwa mahitaji ya maji katika vijiji hivyo ni lita za ujazo milioni 499.5 kwa mwaka, lakini bwawa hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo na kuhifadhi lita bilioni 2 za maji kwa mwaka.
‘Huu mradi ni mkombozi kwa wakazi wa wilaya hii kwani utakapokamilika mbali na kuhudumia eneo kubwa la wilaya pia utakuwa na sehemu maalumu ya kunyweshea mifugo ili kuepusha uharibifu wa vyanzo vya maji, alisema.
Aliongeza kuwa bwawa hilo lenye ukubwa wa ekari 47 ni eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya hifadhi ya chanzo cha maji lakini kutokana na umuhimu wake wakaamua lijengwe kitaalamu ili kuwa chanzo kikubwa cha maji.
Mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi M/S Hematec Investment Ltd kutoka Jijini Dar es salaam ulianza kutekelezwa Agosti 3, 2018 na ulitarajiwa kukamilika Agosti 3, 2019 lakini ukachelewa kutokana na sababu za kiufundi.
Mhandisi Isaac alifafanua kuwa vyanzo vikuu vya maji katika vijiji vyote 18 vilivyoko katika wilaya hiyo ni visima virefu (bore holes) ambavyo havitoshelezi mahitaji, hivyo ujio wa mradi huo utamaliza kero iliyopo katika maeneo mengi.
Alibainisha shughuli zilizokwisha fanyika kuwa ni ujenzi wa tuta, utoro wa maji, birika la kunyweshea mifugo, vituo 2 vya kuchotea maji, ulazaji na ufukiaji mabomba na nyumba ya msimamizi ambapo kiasi cha sh bil 1.5 kimeshalipwa.
Alitaja vijiji 16 vitakavyonufaika kuwa ni Inyonga, Kalovya na Kamalampaka (katika kata ya Inyonga), Utende, Mgombe, Kanoge na Wachawaseme (kata ya Utende), Mtakuja, Nsenkwa na Kaulolo (kata ya Nsenkwa), Ipwaga, Mapili na Masigo (kata ya Ilela) na Kamsisi, Imalaunduki na Songambele (kata ya Kamsisi).
Mwisho
Pichani….Bwawa la Maji la Nsenkwa lililopo katika Kijiji cha Nsenkwa, kata ya Nsenkwa Wilayani Mlele Mkoani Katavi ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 83 na linajengwa kwa gharama ya sh bil 2.9 na kutarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 68,000 wanaoishi Vijiji 16 vilivyoko katika kata 5 za Kamsisi, Utende, Ilela, Inyonga na Nsenkwa.
Attachments area