**********************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAREMBO wa nchi nane wa Miss Jungle International wametembelea machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ili kutangaza zaidi madini hayo.
Warembo hao kutoka Tanzania, Uturuki, Kenya, Hispania, Nigeria, Czchek, Ghana na Guinea, wametembelea kwenye machimbo hayo mji mdogo wa Mirerani.
Mratibu wa Bega kwa bega na Mama Foundation wanaoandaa mashindano ya Miss Jungle International, Martin Rajab amesema warembo hao wametembelea eneo hilo ili kutangaza zaidi madini hayo.
Martin amesema warembo hao nane watashiriki kuwania taji la Duniani kwenye mashindano yatakayofanyika kila mwaka nchini.
“Hawa warembo nane wametembelea machimbo ya madini ya Tanzanite ila washiriki watakuwa 50 kuwania taji la Miss Jungle International,” amesema Martin.
Amesema taji la mrembo wa Miss Jungle International litanakishiwa na madini ya Tanzanite hivyo kuzidi kutangaza zaidi madini hayo duniani.
Miss Jungle International Tanzania Dorine Gibson amesema amefurahia kufika kwenye eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite na kuona sehemu yanapopatikana.
Miss Jungle International Zanzibar, Zuhura Makame amesema watayatangaza madini ya Tanzanite ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour.
Miss Jungle International Kenya, Wendy Wamanga amehoji ni sababu gani madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee na hayapatikani sehemu nyingine yeyote duniani.
Mnyange wa Miss Jungle International Czchek, Sarah Horakova amesema amefurahia kufika kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite kwani amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka kwenye nchi yake kuingia mgodini.
Kaimu ofisa madini mkazi wa Mirerani, mhandisi Castro Maduwa amewakaribisha warembo hao na kuwajulisha kuwa wao wanasimamia mchakato mzima wa uchimbaji, tathimini na uuzaji wa madini hayo.
Mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni ya Franone mining and Gem Ltd, Vitus Ndakize amewaeleza warembo hao kuwa madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee kutokana na jiolojia ya machimbo hayo ilivyokuwa.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tariq Kibwe amesema fursa ya warembo hao kutembelea machimbo ya Tanzanite ni kuzidi kuyatangaza zaidi kimataifa.