Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) wamesisitiza umuhimu wa soko la pamoja katika kukuza
uchumi wakati waliposhiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo maalum wa ngazi ya
Wakuu wa Nchi uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 na mkutano maalum wa ngazi ya
Mawaziri uliofanyika tarehe 20 Julai 2022 jijini Arusha ni sehemu ya mikutano
ya awali kuelekea Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
utakaofanyika tarehe 22 Julai 2022.
Katika mkutano huo Wakuu wa
Nchi walijadili na kuyawekea msisitizo masuala mbalimbali ya hali ya halisi ya
utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki
sambamba na kuainisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa pamoja katika
kuyafikia malengo ya jumuiya hiyo.
Akichangia mada wakati wa
mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
ambaye pia ni mwenyeji wa mkutano huo, amesisitiza juu ya kukuza uzalishaji pamoja
na kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya ili kuweza
kuingia katika ushindani wa kibiashara kimataifa.
Aidha, aliongeza kufafanua
kuwa katika kuyafikia malengo ya pamoja ni muhimu kwa nchi wanachama kuwekeza
katika amani na utawala bora ili nchi ziweze kuongeza nguvu katika usimamizi wa
rasilimali na uzalishaji badala ya kuwekeza katika migogoro.
Naye Mwenyekiti wa mkutano huo
na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta amesisitiza umuhimu wa kuwa na
mawasiliano kupitia ujenzi wa miundombinu ambao ndio msingi mkuu wa kuyafikia
malengo ya soko la pamoja.
Vilevile akaeleza kwa sasa
nchi wanachama zimeunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa na
akatolea mfano ujenzi wa reli ya kisasa unaofanywa na Tanzania ambao
utaziunganisha nchi wanachama na kwamba kwa upande mwingine Tanzania na Kenya
zinaunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu uliofanywa mipakani katika eneo la
Namanga na Taveta.
Maeneo mengine yaliyojadiliwa
ni pamoja na fursa za kiuchumi zilizoongezeka kufuatia Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo kujiunga na jumuiya hiyo, umuhimu wa usimamizi wa rasilimali kama vile
madini na umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuyafikia malengo
yaliyowekwa.
Kadhalika, mkutano huo
ulijadili mafanikio yaliyofikiwa na jumuiya hiyo ikiwemo, uhuru wa kufanya
biashara, mtangamano wa kijamii na fursa za kuvuka mipaka kupitia Hati ya
kusafiria ya kielektroni ya Afrika Mashariki na kuondoleana visa miongozi mwa
nchi wanachama.
Mkutano huo umehudhuriwa na
Nchi zote saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni pamoja mwenyekiti
wa mkutano huo Jamhuri ya Kenya; Mwenyeji wa mkutano huo Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania; Jamhuri ya Uganda; Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya
Sudan Kusini, na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Pia ulihudhuriwa na Jamhuri
ya Shirikisho la Somalia ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika mkutano huo.
==========================================================
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba akifafanua kwa wananchi juu ya umuhimu wa soko la pamoja na fursa zake kwa taifa na wanachi wa Tanzania kwa ujumla kupitia kituo cha Luninga cha TBC1 . |
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akifafanua juu ya fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wananchi kupitia kituo cha Luninga cha TBC1. |
Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakifatilia majadiliano ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika. |
Wapili kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akifuatilia Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.
|