Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya uhuru wa kujieleza kwa raia yeyote wa Tanzania. Katiba hii inampa kila raia haki ya kutoa na kupokea taarifa zinazohusu ustawi wake.
Hata hivyo, haki hii ya kikatiba inakwamishwa na uwepo wa sheria zinazokwamisha uhuru wa watu kujieleza, kupata na kutoa taarifa kupitia vyombo na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano.
Kwa muda mrefu wanahabari na wadau wa habari wameendesha harakati mbalimbali za kuitaka Serikali kuzifanyia marekebisho sheria hizi.
Mojawapo ya sheria zilizolalamikiwa ni Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016, Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 na Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya mwaka 2010.
Pamoja na uzuri wake katika kusimamia haki ya kupata taarifa na kujieleza bado Sheria hizi zina vipengele vinavyokandamiza uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa.
Matumizi ya sheria hizi yamepelekea maamuzi ya kufungiwa kwa magazeti na waandishi wa habari, utozaji wa faini kwa vyombo vya habari, na utoaji wa maonyo kwa vyombo na waandishi wa habari nchini.
Adhabu hizi sio tu zinadumaza uhuru wa kujieleza na kupata taarifa bali pia zinaathiri weledi katika taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Mfano ni kuzorota kwa uandishi wa habari za kiuchunguzi na kuhoji masuala ya msingi, waandishi wa habari kujidhibiti kuandika habari zinazokosoa watawala na kuongezeka kwa uandishi wa habari wa ukasuku.
Baada ya harakati za muda mrefu za wanahabari na wadau wa habari kudai mabadiliko ya sheria za habari na/au vipengele vyake, hatimaye serikali imesikia na kuanzisha mchakato wa marekebisho ya sheria na sera zinayoongoza tasnia ya habari hapa nchini.
Mchakato huu unaowashirikisha waandishi na wadau wa habari unalenga kufanya mapitio na hatimaye kuboresha vipengele vinavyokandamiza uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa.
Hivyo, ni matarajio ya kila mdau wa habari hapa nchini kwamba mchakato huu utapelekea kupatikana kwa sheria nzuri.
Hata hivyo, ni wajibu wa kila mwanahabari na mdau wa habari kushiriki kikamilifu katika mchakato huu ili dhamira ya kupata sheria na sera zitakazolinda na kutetea haki na uhuru wa habari iweze kutimia.