Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt Yahaya Nawanda akizindua moja ya miradi ya maji iliyotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Kijiji cha Msuva kata ya Ngoywa Wilayani Sikonge Mkoani Tabora hivi karibuni kulia kwake ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tabora Mhandisi Hatari Kapufi na kushoto ni Meneja wa RUWASA Wilayani Sikonge Mhandi Fikiri Thomas Samadi.
………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI ya awamu ya 6 imeendelea kumwaga fedha katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maji ili kumaliza kilio cha wananchi katika maeneo hayo.
Miongoni mwa halmashauri hizo ni halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mkoani hapa ambayo imepokea kiasi cha sh bil 2.18 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maji safi ya bomba katika maeneo mbalimbali ili kuboresha upatikanaji huduma hiyo.
Akiongea na gazeti hili hivi karibuni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo Mhandisi Fikiri Samadi alisema juhudi kubwa zinazofanywa na serikali zimewezesha huduma ya maji kufikia asilimia 53.4.
Aliongeza kuwa kiwango hicho cha upatikanaji huduma ya maji safi kinatarajia kuongezeka hadi kufikia asilimia 63 baada ya kuanza kutekelezwa miradi mingine 11 katika kata mbalimbali wilayani humo.
Alibainisha kuwa hadi sasa miradi 5 ambayo imetekelezwa katika kata 4 za Ngoywa, Ipole, Chabutwa na Misheni imekamilika na wananchi wanaendelea kunufaika huku mingine 6 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mhandisi Samadi alifafanua kuwa hadi sasa zaidi ya wakazi 28,000 wilayani humo wanapata huduma ya maji safi na salama ya bomba baada ya kutekelezwa miradi katika maeneo hayo.
Alitaja vyanzo vikuu vya maji katika wilaya hiyo ambavyo vimekuwa msaada mkubwa wa kufikisha huduma hiyo kwa wananchi kuwa ni mabwawa, chemchem na visima virefu.
‘Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea zaidi ya sh bil 2 ili kutekelezwa miradi ya maji katika vijiji mbalimbali, fedha hizi zimetusaidia sana kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali’, alisema.
Aidha alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusaini mkataba wa mradi mwingine mkubwa wa maji unaotarajiwa kutekelezwa katika Miji 28 nchini ikiwemo wilaya hiyo wenye thamani ya zaidi ya sh tril 1.
Alisema ujio wa mradi huo wa maji ya ziwa Victoria ambao utanufaisha wakazi wa vijiji 17 utawezesha upatikanaji wa huduma ya maji safi katika wilaya hiyo kufikia asilimia 85 vijijini na 95 na mjini.