Waziri wa nchi ofisi ya Rais,Zanzibar Jamal Kassim Ali akizungumza katika mafunzo hayo jijini Arusha.
Mwenyekiti wa bodi ya Data Science Afrika (DSA),Dk Ciira Maina akizungumza katika mafunzo hayo yanayofanyika chuo cha uhasibu Arusha .
Mwenyekiti wa bodi ya chuo cha uhasibu Arusha(IAA),Dk Mwamini Tulli akizungumza katika mafunzo hayo chuoni hapo.
…………………………………
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha Zaidi ya wanafunzi 600 kutoka nchi mbalimbali wamefikiwa na elimu juu ya matumizi ya sayansi ya Data ambayo imewawezesha kuongeza ufanisi katika masomo yao na hata kupata ajira kupitia programu hiyo.
Hayo yalisemwa leo jijini Arusha na Mwenyekiti wa bodi ya Mtandao wa wanasayansi wanaofanya utafiti katika maswala ya Data Science Afrika(DSA) ,Dk Ciira Maina wakati akizungumza katika mafunzo hayo yaliyowashirikisha wataalamu wa maswala ya utafiti pamoja na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali yanayofanyika chuo cha uhasibu Arusha.
Dk Maina amesema kuwa,lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki kuwa na uelewa mpana kuhusu maswala ya teknolojia hiyo ya sayansi ya Data na kuweza kuwa suluhisho katika changamoto mbalimbali kwenye jamii ndani ya bara la Afrika.
Amesema kuwa, tayari wameshatoa mafunzo hayo kwa wataalamu mbalimbali katika nchi saba ambazo ni Kenya,Tanzania,Uganda, Ethiopia,Nigeria,Ghana ,na Afrika Kusini ambapo mafunzo hayo yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya,kilimo na mazingira.
“Mafunzo haya yameleta manufaa makubwa Sana katika nchi hizo ambazo tumeenda na kupitia programu hiyo ya Data Science imeweza kuleta matokeo chanya kwa kutatua changamoto mbalimbali katika nchi za Afrika na hata kuongeza fursa za ajira kwa wanafunzi wanaofanya tafiti “amesema Dk Maina
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Zanzibar ,Jamal Kassim Ali amesema kuwa,kitendo cha mafunzo hayo kufanyika jijini Arusha kinaleta fursa kwa wataalamu hao kuweza kufanya mabadiliko katika maeneo yao ya kazi hususani katika maswala ya elimu ya sayansi ya Data .
“kila mmoja wetu anaelewa hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuwa na elimu ya maswala ya sayansi ya data kwa ajili ya uchumi wa juu na wa kati jambo ambalo litasaidia kukuza uzalishaji ,na Kwa kuweza kuanzia ngazi ya wakufunzi watasaidia kuboresha mitaala kwa vijana walioko vyuoni.”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi chuo Cha uhasibu Arusha, Dk.Mwamini Tulli amesema kuwa,chuo hicho kimepata bahati ya kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo ambayo ni muhimu sana kwa uwekaji wa taarifa na yatasaidia sana kuleta mabadiliko chanya kwenye swala la maendeleo kwa nchi za Afrika.
Dk Tulli amesema kuwa, kutolewa mafunzo hayo kwa wataalamu wengi zaidi kutasaidia sana kupata wataalamu wa kutosha katika maswala ya sayansi ya Data ambao watafundisha maswala hayo kwa vitendo zaidi hususuni kwa wanafunzi waliopo vyuoni