Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania, Profesa Makame Mbarawa (kulia) akimkabidhi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa DRC Okende Senga mkataba wa maboresho ya miundombinu mara baada ya mawaziri hao kusaini mjini Kalemie, Nchini DRC.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akikagua miundombinu ya Bandari ya Kalemie wakati alipokuwa ziarani nchini Nchini DRC.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia) katika Picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi wakati alipokuwa ziarani nchini Nchini DRC
PICHA NA WUU
…………………………………………….
SERIKALI za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimetoa mwezi mmoja kwa wataalam wa sekta za ujenzi na uchukuzi kukamilisha taratibu za kupata Mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara ili kuanza kutekeleza miradi hiyo.
Akizungumza mjini Kalemie nchini DRC wakati wa kusaini makubaliano ya awali ya ujenzi huo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa, amesema ni wakati muafaka wa nchi hizo kuunganishwa na miudombinu hiyo ili kuchochea uchumi na kurahisisha shughuli za Uchukuzi baina ya nchi hizo.
“Mkataba huu tuliosaini leo ni mwanzo wa makubaliano ya nchi hizi katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu, hivyo hatua inayofuata sasa ni wataalam kutengeneza hadidu za rejea kuelekea kumpata mkandarasi na kutangaza zabuni” amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema kwa muda mrefu nchi hizo zimekuwa zikizungumza nadharia ya kuboresha miundombinu kwa manufaa ya nchi hizo na kusema ni wakati muafaka sasa wa kuhakikisha mzigo wote unaotoka DRC unasafirishwa kwa wakati kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kutoka DRC, Okende Senga, amesema maboresho ya miundombinu kwa pande zote yatachangia kwa kiasi kikubwa mzigo mkubwa kusafirishwa na hivyo kufanya nchi hizo kuboresha mahusiano ya kibiashara na kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Ushoroba wa kati Central Corridor (CCTTFA), Florian Okanju, amesema kuwa zoezi la kukamilisha hadidu za rejea litakamilishwa kwa wakati kwani imekuwa ni ndoto ya Wakala huo kuona biashara inafanyika bila vikwazo hususani katika masuala ya miundombinu.
Mkataba huo uliosainiwa baina ya Tanzania na DRC unahusisha maboresho ya miundombinu ya reli na barabara yenye urefu wa kilomita takribani 1200 itakayotoka mjini Kalemie mpaka Lubumbashi, uboreshaji wa Bandari ya Kalemie na Momba pamoja na ujenzi wa Meli katika ziwa Tanganyika.