Wakina mama wa Kabila la Wasafwa wakiwa katika maandalizi ya utengenezaji wa pombe ya asili ijulikanayo kwa jina la idadu itakayotumika katika tamasha la utamaduni wa kabila hilo utakaofanyika katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22 hadi 24 mwezi huu. Wakwanza kushoto ni Katibu wa Wasanii wa Kabila kundi la Mbeta Rose Alufani na kulia ni Kristina Mwaniengu ambaye ametumwa na Machifu kwenda kuandaa nyumba za Asili za kabila hiyo kwaajili ya uzinduzi utakaofanyika kesho.
Jiwe linalotumiwa na kabila la Wasafwa linalopatikana mkoani Mbeya kwaajili ya kusaga nafaka mbalimbali lililopo katika nyumba ya kabila hiyo katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mtaalam wa ujenzi wa nyumba za asili za kabila la wasafwa Helena Mwamengo akiendelea na ujenzi ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi wa tamasha la siku tatu la utamaduni wa kabila hilo utakaofanyika kesho katika kijiji cha Makumbusho kilichopo jijini Dar es Salaam.
Mhamasishaji wa tamasha la utamaduni wa kabila la wasafwa kutoka mkoani Mbeya Reddy Makuba akionyesha kamba zinazotumika kufunga mzinga wa kuhifadhia chakula unaotumiwa na kabila hilo linalopatikana mkoani Mbeya.
Mhamasishaji wa tamasha la utamaduni wa kabila la wasafwa kutoka mkoani Mbeya Reddy Makuba (Kushoto) na Katibu wa Tamasha hilo Bahati Mbwete wakionyesha ghala la asili (kihenge) la kuhifadhia nafaka linalotumiwa na kabila hilo linalopatikana mkoani Mbeya.
Wasanii wa kundi la Kabila la Wasafwa kutoka mkoani Mbeya wakiwasili katika viwanja vya kijiji cha Makumbusho kilichopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kushiriki tamasha la utamaduni wa kabila hilo litakalofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 mwezi huu.
Sehemu ya kuishi kaya moja ya kabila la wasafwa ambayo ina nyumba tatu tofauti yenye sehemu ya kuishi familia, kufua chuma, kihenge cha vya kuhifadhia nafaka , boma la ng’ombe na eneo la kufanyia tambiko iliyojengwa katika kijiji cha Makumbusho kilichopo jijini Dar es Salaam.
Picha na Khamisi Mussa
…………………………………..
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Wananchi wa jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wamekaribishwa katika kijiji cha Makumbusho kujionea mila, utamaduni na desturi za kabila la wasafwa.
Mila na desturi hizo zitaonyeshwa katika tamasha la utamaduni wa mtanzania ambapo kabila hilo linalopatikana katika mkoa wa Mbeya litakuwa na siku tatu za kuelezea utamaduni wao.
Ukaribisho huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Wilbard Lema ambaye ni muhifadhi mila mwandamizi wa kijiji cha Makumbusho na mratibu wa tamasha hilo wakati akiongea na waandishi wa habari.
Lema alisema tamasha hilo linalojulikana kwa jina la tamasha la utamaduni wa mtanzania lilibuniwa na bodi ya makumbusho ya Taifa mwaka 1994 kwa lengo la kutoa fursa kwa jamii moja kati ya nyingi zilizopo kwenda katika makumbusho hayo kuonyesha utamaduni wao ili uweze kuhifadhiwa.
“Lengo ni kutambua tamaduni kutoka katika makabila mbalimbali ambazo zitarithishwa kwa kizazi kimoja hadi kingine wakati huohuo kupinga mila potofu ambazo hazifai kuendelezwa”,.
“Makumbusho ya Taifa yanasisitiza wananchi kufanya matamasha ya utamaduni popote pale walipo lakini lengo la kufanya matamasha haya katika kijiji hiki ni kuhifadhi nyumba za asili ambazo zinajengwa hapa kwani nyingi ziko katika hatari ya kutoweka”,.
“Kufanyika kwa matamasha ya utamaduni mahali hapa kunawasaidia watu wa kabila husika ambao wanaishi mjini kukutana na wenzao walioko vijijini na kukumbushana kurudi nyumbani kufanya shughuli za maendeleo”, alisema Lema.
Akizungumza kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili Lema alisema pamoja na Tanzania kuwa na makabila mengi bado taifa linajengwa kwa umoja na mshikamano kwa kuunganishwa na Kiswahili.
Kwa upande wake Bahati Mbwete ambaye ni katibu wa tamasha hilo aliishukuru Serikali kupitia kijiji cha Mkumbusho kwa ushirikiano waliowapa tangu walipoanza kujenga nyumba ya kabila la wasafwa na hadi kufanyika kwa tamasha la mila na utamaduni wa kabila hilo.
Mbwete alisema katika tamasha hilo ambalo halitakuwa na kiingilio chochote kutaoneshwa mambo mbalimbali ambayo yataelezea utamaduni wa asili wa wasafwa hii ikiwa ni pamoja na malezi na makuzi ya familia, vyakula na vinywaji vya asili.
“Katika kijiji hiki tumejenga nyumba ya asili ambayo inaonesha jinsi wasafwa wanavyoishi nyumba hii ni ya kuishi kaya moja ina nyumba tatu tofauti ambayo inasehemu ya kuishi familia, kufua chuma, vihenga vya kuhifadhia nafaka , boma la ng’ombe na eneo la kufanyia tambiko”,.
“Tumefanya tamasha hili na kujenga nyumba hii katika kijiji cha Makumbusho kwa kuwa Serikali imetenga eneo kwaajili ya makabila mbalimbali kujenga nyumba zao za asili na kufanya tamasha ambalo litaeleza mila na utamaduni wao. Baada ya kumalizika kwa tamasha hili nguvu zetu tuzazielekeza mkoani Mbeya ambako tutajenga nyumba kama hii katika eneo la nanenane na kufanya tamasha kubwa”, alisema Mbwete .
Naye Reddy Makuba ambaye ni mhamasishaji wa tamasha hilo alisema wanatarajia kupokea wageni 350 kutoka mkoani Mbeya ambao ni wasafwa kati ya hao kuna vikundi mbalimbali vya ngoma, wazee na machifu 60 wanaotoka katika vijiji ambavyo kabila hilo linaishi.
“Kwa muda wa siku tatu za tamasha hili kutakuwa na mambo mbalimbali yatakayofanyika ambayo yataeleza utamaduni wa wasafwa pia wazee wetu hawa wataelezea asili ya kabila hili ni wapi na jinsi wanavyoishi hii ikiwa ni pamoja na mila na utamaduni wao”, alisema Makuba.
Naye Akwilina Mbaza kutoka mkoani Mbeya alishukuru kuwepo kwa tamasha hilo ambalo litatangaza mila na utamaduni wa kabila la wasafwa na hivyo kuwafanya watu wengi kujifunza na kulifahamu kabila hilo linalopatikana katika mkoa huo.
“Wasafwa ni watu wapole na wakarimu wenye umoja na mshikamano pia wanapenda watu, kwa asili wasafwa ni wakulima na wanajituma kufanya kazi. Ninawaomba watanzania wafuate mila zao kwani hivi sasa kuna watu ambao wameacha kudumisha mila zao na kufuata mila za kigeni ambazo kwa kiasi kikubwa zinawaharibu na kuwatoa katika uasili wao”, alisema Akwilina.
Tamasha hilo la siku tatu litafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 24 mwezi huu katika kijiji cha Makumbusho kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam litafunguliwa kesho na waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana.