NA VICTOR MAKINDA: NZEGA
Kasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha kila mmoja anafaidi keki ya Taifa kwa kufikiwa na maendeleo imetua wilayani Nzega mkoani Tabora.
Hayo yameelezwa leo na Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijiji Nchini (TARURA),wilayani Nzega, Injinia Haruna Mbagalla, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu uwekaji wa taa za barabarani sambamba na ujenzi wa barabara mpya za lami mjini Nzega.
“ Kasi kubwa ya ujenzi wa barabara mahali pote nchini hususani wilayani Nzega ni matunda yanayotokana na dhamira njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kuwa maendeleo yanawafikiwa wananchi wote nchi nzima mijini na vijijini.” Alisema Mbagalla.
Mbagala alibainisha kuwa TARURA imekwisha anza kazi ya ufungaji wa taa kwenye barabara za Nzega mji na tayari zimefungwa taa 16 huku wakitaraji kufunga taa nyingine 18 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022-23.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa barabara za lami Nzega mjini, Mbagalla alisema kuwa TARURA inataraji kujenga barabara za lami zenye urefu wa Kilometa 2 kwa mwaka huu wa fedha, ambapo ujenzi huo utakwenda sambamba na uwekaji wa taa huku wakiwa na matarajio ya kupata mradi wa TACTIC kutoka Benki ya Dunia ambapo jumla ya kilometa 9 za lami zitajengwa na kuweka taa.