*************************
Na Silvia Mchuruza.
Karagwe, Kagera
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amekerwa na kasi ndogo ya ujenzi wa Shule mpya ya wasichana ya Mkoa Kagera na kumuagiza Mkandarasi kukamilisha kazi ndani ya miezi minne.
Bashungwa ameyasema hayo Julai 19, 2022 mara baada ya kujionea utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule mpya ya wasichana ya Mkoa Kagera inayojengwa eneo la Rwaimbaizi Kata ya Kituntu.
Shule hiyo inayopendekezwa kuitwa Shule ya Sekondari Kagera River.
Waziri Bashungwa amemtaka mkandarasi kuongeza nguvukazi na kuanza kuamusha majengo yote kwa wakati mmoja bila kusubili kumaliza majengo ya awamu ya kwanza ndipo aanze ujenzi wa majengo ya awamu ya pili.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaleta shilingi bilioni 3 zote zipo kwenye akaunti, alafu nyie mnaanza kujenga kwa awamu mbili, masuala ya kuleta sababu kuwa ukamilisha wa majengo utategemeana na hali sitaki kuyasikia, umepewa mkataba wa miezi minne ikiisha nitakuja mwenyewe kukagua,” amesema Bashungwa
Waziri Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameuwezesha Mkoa wa Kagera kwa kuupatia kiasi cha Sh bilioni 3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ili mwakani ianze kupokea wanafunzi.
Pia amemuagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kuhakikisha kila siku inasimamia kwa ukaribu ujenzi wa shule hiyo ili majengo yote yakamilike kwa wakati bila kuathiri viwango vya kitaalam.
Waziri Bashungwa amesema Mkandarasi anatakiwa kukamisha kazi hiyo Septemba 8 mwaka huu na kuahidi kufika tena kwa ajili ya kukagua mradi huo kama umeisha na unaendana na thamani ya fedha aliyolipwa.
Kwa Mujibu wa Mkataba Ujenzi utafanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 16, awamu ya pili ni ujenzi wa majengo la utawala, mabweni matano, nyumba mbili za walimu, vyoo, kisima cha maji na uzio wa shule.