Na Mwamvua Mwinyi, KIBAHA
KIASI Cha sh.Milioni 68 za Mfuko wa Jimbo Kibaha Vijijini, Mkoani Pwani zilizotolewa kwenye vipindi viwili zimewezesha kuanzisha ujenzi wa shule tatu za Sekondari jimboni hapo, ili kuinua na kuboresha sekta ya elimu.
“Milioni 34 za kwanza nilianzisha shule ya Sekondari Disunyara, Serikali ikaongeza madarasa sasa yapo zaidi ya kumi, pia nikaanzisha shule mbili mpya za Kawawa nayo imepokea wanafunzi, hivi sasa sekondari ya tatu imeshaanza kujengwa Boko,”
Mafanikio hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo hilo , Michael Mwakamo, wakati wa ziara yake ya kuzungumza na baadhi ya Wakazi wa vitongoji ,Jimbo la Kibaha Vijijini.
Mwakamo Alifafanua, Matumizi mazuri ya fedha za Mfuko wa Jimbo wa sh. milioni 68 kwa vipindi viwili, yamembeba ambapo kwasasa ameongezewa sh.milioni 20.
Alieleza ,kuongezwa kwa kiasi hicho cha fedha sasa kinaliwezesha jimbo kupokea sh.milioni 54 kwa mwaka, kutoka milioni 34 zilizokuwa zinapokelewa kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi.
“Nikiwa bungeni niliomba Serikali iniongezee fedha za mfuko wa Jimbo, lakini niliambiwa jimboni kuna watu 70,000 hivyo milioni 34 zinanitosha,nikawaomba watembelee miradi niliyoitekeleza katika kipindi changu cha ubunge ,wakajionea namna nilivyozitendea haki fedha zile na Sasa nashukuru ,fedha zimeongezwa naamini tutafanya makubwa “.
Alieleza, baada ya Serikali kutuma watu wake jimboni na kujionea ,waliridhishwa na matumizi ya mfuko huo na Sasa tumeongezwa kiasi cha shilingi milioni 20, hivyo mfuko huo utakuwa unapokea sh. milioni 54 kila mwaka.
“Pamoja na mafanikio yote ambayo sijayazungumza yote , niwaombe wananchi wenzangu tujiandae kikamilifu kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi, linalotarajia kufanyika agost 23 mwaka huu, sensa imeandaliwa na Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu inalengo la kutambua watu wake ili ipange vizuri mipango yake,”Twende tukajitokeze kutimiza azma hii, alihimiza Mwakamo.