Katika kuhakikisha timu za daraja la kwanza Tanzania bara na timu za ligi daraja la pili zinapata mechi za kujifua ili kujiandaa na msimu mpya, Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza MZFA kwa kushirikiana na Kampuni ya Fraki wamekuandalia michuano ya Utalii Cup 2022 itakayofanyika katika jiji la Mwanza.
Katibu Mkuu wa MZFA Mwalimu Leonard Charles Malongo amesema wameamua kuandaa michuano hiyo lengo likiwa ni kuziwezesha timu mbalimbali ambazo zitashiriki katika za kujipima nguvu Kuelekea kwenye msimu wa ligi mbalimbali nchini Tanzania.
“Tumeamua kuandaa kombe la Utalii Cup 2022 kwa sababu mbalimbali, moja ikiwa ni kuvipa nafasi vilabu mbalimbali kucheza ili kujipima nguvu mapema kabla kuanzia ligi ambazo zinatambulika na TFF na Bodi ya ligi, ligi ambazo zinatarajia kuwa ngumu kupita msimu uliopita”
“Kusudi lingine ni kutangaza vivutio vya Utalii vilivyoko katika maeneo mbalimbali katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kama vile Saa Nane National Parks, Serengeti, Rubondo, Burigi Chato na Bujora. Michuano hii itatoa fursa kwa watu mbalimbali kwenda kuangalia Utalii wa ndani kama inavyohimiza Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan”
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Fraki Francis Shao ambao ndio waratibu wa michuano hiyo amesema wanafarijika kuona Chama cha Soka Mkoa Mwanza MZFA wameipokea michuano hiyo vizuri na kuipa heshima ya kutosha.
“Sisi ni waratibu tu ila wanaoandaa ni MZFA, ukweli tumeona mwitikio mkubwa toka tuamue kuleta mashindano hayo Mwanza. Kikubwa tunaomba timu mbalimbali na za ligi kuu kujitokeza zishiriki ili kujipima nguvu kujua wapi walipo bora na wapi walipo dhaifu ili warekebishe” alisema Shao.
Mshindi wa kwanza kwenye michuano hiyo atapata zawadi shilingi milioni tano kombe na medali, mshindi wa pili atapata shilingi milioni tatu na medali, mshindi wa tatu atapata shilingi milioni moja na nusu na wa nne atapata zawadi ya shilingi laki tano.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanzia kurindima katika uwanja wa Nyamagana na CCM Kirumba kuanzia 27 Julai mwaka huu hadi tarehe 12 Agosti mwaka huu. Hadi sasa timu sita zimethibitisha kushiriki ingawa bado nafasi ipo kwa timu kuongezeka.