Katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki ,Peter Mathuki akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha juu ya ujio huo.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela akizungumza katika kikao hicho na waandishi wa habari jijini Arusha leo.
************************
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha .WAKUU saba wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wanatarajiwa kuwasili Jijini Arusha kuanzia kesho kwa ajili ya kushiriki mkutano wa 22 wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.
Aidha kabla ya kuanza kwa kikao hicho wakuu hao watashiriki kwa pamoja uzinduzi wa barabara ya East Afrika By pass ambayo imejengwa kwa fedha za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na serikali ya Tanzania.
Pia amesema mkutano huo utakuwa wa kipekee kwa sababu itakuwa ni wa mara ya kwanza kwa nchi ya Demokrasia ya Congo kushiriki baada ya kupokelewa rasmi hivi karibuni.
Akizungumza kwenye makao makuu ya Jumuiya hiyo Jijini Arusha,Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Dk,Peter Mathuki amesema mkutano huo wa wakuu wa nchi za EAC utakuwa wa kwanza tangu janga la Covid 19 lilipoikumba Dunia kwa kuwa wakuu hao walikuwa wanafanya vikao kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa Dk Mathuki amesema kikao hicho kutafanyika Julai 21 hadi Julai 22 mwaka huu ambapo ajenda mbalimbali zitajadiliwa.
“Kikao hiki cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni cha kawaida na kitakuwa na ajenda mabalimbali ikiwemo namna bora ya kujiendesha kwa manufaa ya wananchi wa nchi wanachama pamoja na namna bora ya kutatua changamoto zinazoikabili Jumuiya yetu”.amesema .
Kuhusu ulinzi na usalama mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha hali ya amani na utulivu inatawala muda wote ambao viongozi hao watakuwa katika Jiji la Arusha.
Akizungumzia uzinduzi wa barabara ya East Afrika By Pass Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema uzinduzi wa barabara hiyo utafanyika eneo la Mringa Estate Ngaramtoni majira ya saa mbili asubuhi na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo.
“Tumejipanga kikamilifu kuwapokea wakuu hawa wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki wanaokuja katika mkoa wetu kwa ajili ya mkutano wao wa kawaidia lakini pia kushiriki uzinduzi wa barabara ambayo Jumuiya hiyo itoa kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania”amesema.