MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utendaji kazi wa RUWASA.
MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo Julai 19,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utendaji kazi wa RUWASA.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari wakati wa taarifa ya utendaji kazi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) leo Julai 19,2022 jijini Dodoma .
…………………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI kupitia wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa mwaka wa fedha 2022 – 2023 inatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 387.73 kutekeleza jumla ya miradi ya maji 1,029 nchi nzima ambapo kati ya miradi hiyo 381 ni mipya na miradi 648 ile ambayo utekelezaji wake unaendelea kutoka mwaka wa fedha uliopita.
Kutolewa kwa shilingi bilioni 387. 7 kunafanya kufikia zaidi ya shilingi bilioni 889.2 fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani katika kumaliza kero ya maji katika maeneo ya vijijini.
Hayo yamebainishwa leo Julai 19,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji Vijijini kupitia bajeti ya 2022 – 2023 ambapo amesema kiasi hicho ni kikubwa kuwahi kutolewa na kuahidi kusimamia kikamilifu kumaliza kero ya maji Vijijini.
“Kiasi cha bilioni 387,736,591, 242 hizi ni fedha ambazo zimeidhinishwa na Bunge kwa ajili utekelezaji wa miradi hiyo kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma za maji vijijini na kuongezeka kwa wastani wa asilimia 6” amesema Kivegulo.
Akizungumzia kupeleka maji katika kijiji cha Msomera Handeni Tanga amesema RUWASA inaendelea na ujenzi wa bwawa la maji katika kijiji cha Msomera kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.99 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 15 na Ujenzi huo utakapokamilika, utasaidia kuboresha huduma ya maji kwa wananchi pamoja na mifugo.
RUWASA inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji hicho, ambapo mpango wa utekelezaji uligawanywa katika awamu mbili (awamu ya muda mfupi na awamu ya muda mrefu),Ambapo awamu ya muda mfupi imekamilika na vituo vya kuchotea maji 12 vimeshaanza kutoa huduma ya maji, awamu ya pili imefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2022.
Amesema kukamilika kwa awamu hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 17,000 pamoja na mifugo yao na kupelekea idadi ya vituo vya maji kuongezeka kutoka 12 hadi kufikia vituo vya kuchotea maji 30 kwa matumizi ya binadamu na vituo 3 vya kunyweshea maji mifugo.
“Niwahakikishie tu wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera kuwa hawatapata changamoto yeyote ya maji hivyo ambao bado hawajahamia wafanye hivyo kwa uhakika RUWASA imedhamiria kuondoa kabisa tatizo la maji katika vijiji vyote na kusaidia kukamilisha adhma ya Mhe.Raisi ya kumtua mama ndoo Kichwani”amesema Mhandisi Kivegalo
Mhandisi Kivegalo amesema kuwa kwa sasa, kati ya vijiji vyote nchini 12,319 ni vijiji 8,769 vinavyofikiwa na huduma ya uhakika ya maji safi na salama.
“Kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika mwezi Aprili, 2022 upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ulikuwa umefikia kiwango cha asilimia 74.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.7 ikilinganishwa na wastani wa 64.8 mwaka 2019″Amesema Mhandisi Kivegalo
Na kuongeza “Kasi hii, ni nzuri na tukienda kwa kasi hii, tunatarajia kuvuka lengo la asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi”
Ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia RUWASA ilipanga kutekeleza jumla ya miradi ya maji 1,527, ambapo kati ya hiyo, miradi 1,176 ilikuwa ni ujenzi wa skimu za usambazaji maji, miradi 351 ilikuwa ni ya utafutaji wa vyanzo vya maji chini ya ardhi na miradi 19 ilikuwa ni ya usanifu na jenzi wa mabwawa, ambayo baadaye hutumika kama vyanzo vya maji.
Mhandisi Kivegalo ameeleza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya miradi 303 ilikuwa imekamilika na miradi 873 ilikuwa inaendelea na utekelezaji,Miradi 225 kati ya miradi iliyokuwa inaendela na utekelezaji inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2022 na miradi 648 itaendelea na utekelezaji. Kukamilika kwa miradi 303, kumewezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 1,467,107 kupitia vituo vya kuchotea maji 4,147 vilivyojengwa katika maeneo ya vijiji mbalimbali.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa katika sekta ya maji Mhe.Rais ameahidi na anaendelea kutekeleza kauli mbiu yake ya kumtua mama ndoo kichwani kwa sababu bila maji hakuna jambo lolote la kijamii au kimaendeleo linaloweza kuendelea ndio maana RUWASA wanapambana usiku na mchana kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya maji kwa uhakika.
“Kwanza niwapongeze RUWASA kwa sababu tangu kuanzishwa kwa mamlaka hii imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kuhakikisha vijiji ambavyo hawakuwa na huduma za maji vinapata maji na kwa kweli kazi yenu inaonekana na matokeo yake imemfanya Mhe.Rais kuongeza bajeti ya wizara ya maji ili kuendelea kuongeza tija ya upatikanaji wa maji kwa wananchi “Amesema Msigwa.