************************
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Anthony Mtaka ametaka wadau wote kuungana pamoja kuhakikisha sekta ya michezo mkoani Dodoma inakua na kurejesha sifa ya Dodoma kitaifa katika michezo.
Mh Mtaka ameyasema hayo jana wakati akifungua mkutano mkuu wa Umoja wa Familia wa Wanamichezo wa Zamani(UFAWAZA) katika Hoteli ya Royal Village Dodoma kwa kuwataka wadau wote wa michezo mkoani Dodoma kuunganisha nguvu ili kuinua michezo mbalimbali mkoani Dodoma.
“Niwapongeze UFAWAZA kwa kuwa na maono mazuri ya kutengeneza umoja huu wa wwchezaji wa zamani wenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali na kusaidia kukuza michezo hapa mkoani Dodoma.
Katika Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA nitahakikisha ninatoa wataalamu kutoka familia hii kwenda kuchagua wachezaji wenye vipaji ili tuwaendeleze na kuwakuza.
Nakupongeza Mavunde kwa kuusaidia huu umoja kwa hali na mali na pia kwa kuwa karibu na Timu yetu ya Dodoma Jiji kwa kipindi kirefu.
Kwa kuwa kwasasa umeweka nguvu kwenye mashindano ya NDONDO CUP na kuaga rasmi huku Dodoma Jiji,sisi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa sasa tutaisimamia timu hii ya Dodoma Jiji kwa ushirikiano na Jiji la Dodoma ili ziwe miongoni mwa timu zitakazofanya vizuri katika ligi msimu ujao”Alisema Mtaka
Akizungumza katika mkutano huo,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amesema kwa sasa mtazamo wake ni kukuza vipaji vya wanadodoma kupitia mashindano ya Ndondo Cup na atasaidia kurekebisha miundombinu ya viwanja vya michezo vingi Jijini Dodoma kwa kuweka magoli ya chuma na kupitisha mitambo ya kuvifanya viwanja vichezeke kwa urahisi.
Naye Mwenyekiti wa UFAWAZA Bwana. Ally Kheri* ameeleza kuwa malengo mahsusi ya familia ya wana michezo hao ni kwanza kutambuana na pia kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanamichezo wa zamani na kutoa rai kwa wanamichezo wa zamani wa Dodoma kujiunga na familia hiyo.