Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, (katikati) akizungumza na Wakaguzi wa Afya wa OSHA wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha kutathmini utendaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka kwa fedha wa 2021/2022 pamoja na kupitia miongozo na kanuni mbalimbali za afya mahali pa kazi kilichofanyika jijini Dodoma.(Pembeni yake) ni viongozi mbalimbali wa menejimenti ya OSHA.
Mkurugenzi wa Mfunzo, Utafiti,Takwimu na Uhamasishaji, Bw. Joshua Matiko akizungumza na Wakaguzi wa Afya wa OSHA wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi kiilicho fanyika jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa OSHA, Bi. Netiwe Mhando.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (katikati) akionyesha kwa Wakaguzi wa Afya wa OSHA kitabu cha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Taasisi ya OSHA katika Kikao Kazi kiilicho fanyika jijini Dodoma.
Wakaguzi wa Afya wa OSHA wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Kikao Kazi iliyowasilishwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.
**********************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeelezea nia yake ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia uimarishaji wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwafanya wawekezaji wajisikie fahari kuwekeza nchini.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, wakati akifungua Kikao Kazi cha siku tano jijini Dodoma kilichowakutanisha Wakaguzi wa Afya wa OSHA kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Wote tunaona mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyosisitiza namna ya kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kufanya biashara nchini hivyo kupitia kikao kazi hiki sisi OSHA ambao ni Taasisi wezeshi tunaangalia ni namna gani ambavyo tunaweza kuwezesha mazingira ya uwekezaji na baishara nchini yakawa ni rafiki zaidi hivyo kuwafanya wafanyabishara na wawekezaji wajisikie fahari kuwekeza nchini” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda nakuongeza:
“Tumekaa na timu ya madaktari wa OSHA wapatao mia moja nia na madhumuni kwanza ni kuhakikisha tunatoa huduma bora na kwa wakati lakini pia tunaangalia ni namna gani tutawezesha maeneo ya kazi nchini yaweze kusimamia Sheria Namba 5 ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi ya Mwaka 2003.”
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA, Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika siku za hivi karibuni limepitisha azimio la kila nchi mwanachama ahakikishe anasimamia kikamilifu masuala ya usalama na afya kazini jambo ambalo limepelekea Taasisi yake kuanza kujipanga kutimiza azimio hilo la ILO.
Kwa upande wao wakaguzi wa afya wa OSHA wamesema kuwa baada ya kikao kazi hicho kumalizika watakuwa na maono ya pamoja katika kuboresha mazingira ya kazi nchini huku wakitoa wito kwa kwaajiri kusimamia ipasavyo Sheria Namba.5 ya Usalama na afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003 ilikuleta tija katika uzalishaji.
“Kupitia kikao kazi hiki tutatoka na maazimio ya pamoja yatakayotuongoza katika kuboresha mazingira ya kazi hivyo kila mmoja wetu akitoka hapa atakuwa anajua malengo ya Taasisi ni yapi mathalani tunahitaji kuwafikia watu wangapi na tutafanya kazi kwa kiasi gani katika mwaka mpya wa fedha wa 2022/23,” amesema Dkt. Denis Gabriel amabye ni Mkaguzi wa Afya wa OSHA.
Naye Blandina Reuben ambaye ni Mkaguzi wa Afya wa OSHA, amewataka waajiri kusimamia ipasavyo sheria na miongozo mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuleta tija katika uchumi wan chi yetu.
“Nitoe wito kwa waajiri wote katika maeneo mbalimbali ya kazi wazingatie Sheria Namba 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003 kwasababu sheria hiyo ikizingatiwa ipasavyo inampunguzia gharama mwajiri na kuongeza tija katika eneo la kazi” amesema Blandina.
Kikao kazi hicho kinafanyika kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na kupitia miongozo na kanuni mbalimbali za afya mahali pa kazi ili kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hiyo.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye jukumu la kusimamia Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama na Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba shughuli zote za uzalishaji nchini zinafanyika kwa kuzingatia taratibu za afya na usalama ili kulinda nguvukazi na mitaji ya wawekezaji.