Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Kamati ya sensa wilayani humo Sunday Deogratias amesema usahili wa waombaji wa zaoezi la sensa utafanyika kwa uwazi na haki pasipo kupendelea upande wowote bali watakao onekana kuwa na sifa ya kufanya kazi hiyo ndio watakao patiwa ajira.
Akiyasema hayo katika kikao cha kamati ya sensa kwa niaba ya mkuu wa wilaya ambaye ndiye mwenyekiti Deogratias amesema kuwa usahili huo unatarajiwa kuanza julai 19 hadi 21 mwaka huu katika makao makuu ya kila kata walikoombea hivyo waombaji wote ambao majina yao yametolewa wametakiwa kufika na vyeti vyao vya taaluma pamoja na nakala zake.
“Kumekuwa na maneno maneno katika maeneo mengi kuwa ajira za sensa zinatolewa kwa kujuana na upendeleo, katika halmashauri yangu hicho kitu hakiwezi kutokea bali tutahakikisha wanaopata ajira ni wale waliokidhi vigezo na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi”, Amesema Mkurugenzi.
Aidha kwa upande wa mratibu wa sensa wilayani Ludewa Alex Henjewele amesema maombi yaliyo wasilishwa ni 2130 ambapo miongoni mwa waombaji hao 250 hawakukidhi vigezo kwa kutowasilisha baadhi ya fomu na kupelekea kubakiwa na waombaji 1880 huku idadi ya wanaohitajika ikiwa ni 668.
Henjewele ameongeza kuwa Sambamba na hao ambao hawakukidhi vigezo lakini pia kuna baadhi ya waombaji 38 wakiwemo maafisa elimu ambao nao waliomba wameondolewa na kupewa majukumu mengine ambapo tayari wamekwisha anza kupatiwa mafunzo na yanatarajiwa kukamilika julai 26 mwaka huu na kupelekea kubakiwa na idadi ya majina 1842.
“Watu wanaohitajika katika zoezi hili ni 668, makalani 582, wasimamizi wa maudhui 60 na maafisa tehama 26 hivyo baada ya kufanya usahili na kupata idadi hii ya watu julai 29 hadi Agosti 18 watapatiwa mafunzo tayari kwa kuanza kazi”, Amesema Henjewele.
Zoezi hili la Sensa linatarajiwa kuanza kufanyika Agosti 23 mwaka huu kote nchini ambapo wananchi wote wanatakiwa kushiriki zoezi hili kikamilifu ili kujipatia maendeleo.