Wakandarasi nchini wameiomba Serikali kuendelea kusaidia kupunguza kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol na dizeli ili waweze kumaliza miradi yao kwa wakati.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Wakandarasi Wazalendo nchini (ACCT), Thobias Kyando wakati wa Mkutano wa 11 wa Mwaka wa chama hicho uliofanyika leo jijini Dodoma.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa wakandarasi wengi waliingia makubaliano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mwishoni mwa mwaka jana kabla bei ya mafuta ya petroli na dizeli hazipanda.
“Wakandarasi wazawa wameathirika sana kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta. Wakati tunasaini makubaliano ya miradi mbalimbali mwaka jana kwa mfano bei ya mafuta ya dizeli kwa mkoa wa Dodoma ilikuwa tsh 2300/- lakini hivi sasa imefika tsh 3200/-.
Utekelezaji wa miradi wa miradi umekuwa ni mgumu na wengi wameshindwa. Tunaishkuru serikali kwa jitihada inayoendelea nazo za kuhakikisha bei hii haipandi sana na tunawaomba waendelee kutoa zuruku ili bei iweze kushuka vingenevyo wengi watashindwa kuimaliza hii miradi au wataimaliza kwa shida sana,” ameshauri mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACCT, Samwel Marwa amesema kuwa dhumuni la kuanzishwa kwa chama hicho ni kutetea maslahi ya wakandarasi wazawa huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuwapa kipaumbele pamoja na kuboresha sera ambazo zinawajumuisha wakandarasi wazawa katika miradi mbalimbali nchini.