Mwenge wa Uhuru ukiwasilia eneo la mradi wa mfumo Rahisi wa Uondoaji wa majitaka katika Makazi ya Miinuko Sahara Igogo, wilayani Nyamagana leo. Meneja miradi wa MWAUWASA na msimamizi wa mradi wa Mfumo Rahisi wa uondoaji Majitaka katika Makazi ya Miinuko, Mhandisi Celestine Mahubi (kushoto) akitoa taarifa ya mradi huo leo.
NA BALTAZAR MASHAKA,Nyamagana
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Sahili Geraruma,ameridhishwa na Mradi wa Mfumo Rahisi wa Uondoaji wa Majitaka katika Makazi yenye miinuko (milimani) ,Sahara Igogo ((Simplified Sewerage System) jijini Mwanza.
Pia ameiongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kwa kutekeleza mradi huo vizuri na kuigiza kuutanua zaidi na kuupeleka katika maeneo mengine ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi ili kudhibiti utiririshaji wa majitaka ovyo.
Akizindua mradi huo leo , Gereruma alisema mradi huo umetekelezwa vizuri, kwa viwango na ubora utakaolifanya Ziwa Victoria na Wilaya ya Nyamagana kuwa safi na salama.
“Mradi huu ni mzuri sana kwa namna ulivyotekelezwa na naagiza MWAUWASA upelekeni maeneo mengine uwanufaishe wananchi wengine zaidi,sasa wakazi wa milimani tabia ya kuzibua vyoo wakati wa mvua haipo tena, jiungeni kwenye mfumo huu,” alisema.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa uhuru aliwataka wananchi kabla ya kujenga nyumba za makazi katika maeneo ya milimani wapate ushauri na maelekezo kutoka MWAUWASA ya ujenzi wa miundombinu ya makazi na majitaka.
Awali Meneja Miradi na Msiamamizi wa mradi huo Mhandisi Celestine Mahubi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Mhandisi Leonard Msenyele, alisema mradi Sahara Igogo utaondoa na kupunguza utiririshaji wa majitaka kutoka majumbani kuelekea ndani ya Ziwa Victoria.
Alisema utirishaji ovyo wa majitaka unaofanywa na wakazi wa milimani (miinuko) umekuwa ukisababisha uchafuzi wa maji ya Ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikuu cha kikubwa cha maji kwa wananchi na wakazi wa mwambo wa ziwa hilo na Jiji la Mwanza.
“Ujenzi wa mradi wa Mfumo Rahisi wa uondoaji wa majitaka katika Makazi ya Miinuko katika maeneo ya Ibungilo,Kabuhoro, Isamilo na Igogo-Sahara,ulianza kutekelezwa Juni 23, 2020 na mkandarasi Whitecity International Contaractors ltd kwa usimamzi wa MWAUWASA na kukamilika juni 24, mwaka huu ,”alisema mhandi Mahubi.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania pamoja na wadau wa maendeleo, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa mkopo wa masharti nafuu.
Mhadi Mahubi alisema mradi wa Sahara Igogo pekee hadi kukamilika umegharimu sh.887,047,312.50 huku maeneo yote manne ya miradi ya Kabuhoro,Ibungilo,Isamilo na Sahara Igogo yakigharimu jumla ya sh.3,844,768,482.50.
Alifafanua kuwa mradi wa Sahara ulihusisha ulazaji wa bomba la urefu wa km 5.56, ujenzi wa chemba kuu 315 za kukusanyia majitaka zilizounganishwa katika bomba kuu,,chemba ndogo 393 za majumbani.
Pia kaya 393 zimeunganishwa katika mfumo huo wa majitaka,vyoo 33 vilivyokuwa katika hali mbaya vimeboreshwa kuruhusu uunganishwaji wake katika mfumo,ujenzi wa njia na uboreshaji wa mfumo wa usambazaji wa majisafi ambapo kaya 122 ambazo hazikuwa katika mfumo huo wa majisafi zimeunganishwa .
“Kupitia mradi huu kaya 393 katika mfumo wa majitaka ambapo jumla ya wakazi 2,358 wa eneo la Sahara Igogo,wamenufaika na huduma ya mradi huu ambao umeondoa ama kupunguza utiririshaji ovyo wa majitaka kuelekea ndani ya Ziwa Victoria, hivyo kulinda usalama wa maji kutokana na uchafuzi unaosababishwa na jami kutiririsha majitaka pia umepunguza magonjwa ya kipindupindu, kichocho, kuhara na homa ya matumbo,” alieleza mhandisi Mahubi.
Naye Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, kwa niaba ya wananchi alimshukuru Rais Samia kwa kuwezesha fedha za kutekeleza mradi huu kwa wakazi wa milimani na kuomba uwezeshaji zaidi ili kuboresha miundombinu ya majitaka kwa wananchi waishio milimani ili kuondokana na magonjwa.