*************************
Jamii imetakiwa kuwafichua watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum Ili nao washiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia mwezi Agosti 23, mwaka huu
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na Wanawake wa Mkoa wa Mwanza katika ukumbi wa City Link kata ya Buswelu juu ya kushiriki Zoezi la Sensa, kupinga vitendo vya ukatili, kupokea taarifa ya hitimisho la Bunge la bajeti na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ambapo amewataka kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika fursa mbalimbali zinazojitokeza katika jamii pamoja na kuingizwa katika mipango ya maendeleo ya Serikali kupitia Sensa
‘.. Tuwafichue watu wenye ulemavu na ikitokea mmoja wetu amemficha basi jamii itimize wajibu wake kumfichua, Si tunajuana tunavyoishi katika maeneo yetu ..’ Alisema
Aidha amewataka kumshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Wizara maalum inayosimamia makundi maalum na jinsia jambo linalosaidia kupunguza vitendo vya kikatili katika jamii huku akimpongeza Waziri husika Mhe Dorothy Gwajima Kwa namna anavyojitoa Kila akisikia vitendo vya ukatili katika jamii
Kwa upande wake mkurugenzi wa taasisi ya Kivulini iliyopo kata ya Nyamhongolo Bwana Yasin ameiasa jamii kutochagua aina ya uovu wa kukemea huku akitolea mfano wa mwizi anapoiba hata kitu chenye thamani ya shilingi mia tano jamii inamchoma moto Ila anaelawiti au kutelekeza familia akiachwa huru bila hatua zozote kuchukuliwa
Nae mratibu wa sensa kwa manispaa ya Ilemela Ndugu Yohana Magesa amesema kuwa sensa ya mwaka 2022 ni ya tofauti na sensa zote za miaka ya nyuma kwani haitatumia mfumo wa ujazaji wa madodoso ya karatasi badala yake itatumia teknolojia ya kishikwambi na ni ya kisayansi zaidi huku akiwasisitiza wananchi kushiriki Ili kupata takwimu sahihi zitakazotumika katika mipango ya maendeleo ya Serikali
Mchungaji Joyce Mangu ni miongoni mwa Wanawake walioshiriki kikao hicho ambapo amempongeza na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Kwa uamuzi wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya jamii yanayopatikana ndani ya Jimbo lake kuhamasisha ushiriki wa Sensa, kutoa fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo huku akiwataka viongozi wengine kuiga mfano huo.