*Wadai
kuna vigogo wanaoratibu zoezi zima la uvamizi wa ardhi, wahatarisha maisha ya
wenye hati miliki za ardhi, wafyeka mazao na mifugo.
Na
MWANDISHI WETU
Wamiliki
ardhi kata ya Mabwepande Wilaya ya Kindondoni waililia serikali kuwaondoa
wavamizi wa ardhi wanaohatarisha usalama katika maeneo hayo. Suala la uvamizi
wa ardhi limezua hali ya sintofahamu kwa wamiliki kwani wavamizi hao
wanaonekana ni kama genge linaloratibiwa na vigogo, hayo yameelezwa na wamiliki
leo Mabwepande, Kinondoni Dar es salaam.
Wakizungumza
na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baadhi ya wananchi ambao ardhi zao
zimevamiwa walisema chanzo cha uvamizi wa ardhi ni watu waliokuwa wanachimba
kokoto miaka 2000 ambao walianza kuvamia eneo la Nyakasanga na kujikatia
viwanja kwenye maeneo ya watu.
Mzee
Pascha Lutege alisema eneo lake alinunua mwaka 1995 na alianza kufunga ng’ombe
na mbuzi ambapo mwaka 2008 alianza kulipima eneo lake na ilipofika mwaka 2012
upimaji ulikuwa umekamilika na alipata hati ya kumiliki ardhi.
“Nilikuwa
nimejenga nyumba, banda la ng’ombe, banda la mbuzi, nilikuwa na tofali zaidi
3,500 na nilikuwa nimechimba bwawa kubwa kwa ajili ya kufuga samaki, lakini
wavamizi wa ardhi walikuja wakavamia eneo langu lote na kufanya uharibifu
mkubwa kwa kupora ng’ombe, mbuzi, walibomoa nyumba na kumkata mapanga kijana
aliyekuwa anaishi eneo hilo pamoja na kuvuruga bwawa la samaki,” alisema.
Mzee
Lutege alisema mwaka 2011 alifanikiwa kuwakamata waliovamia katika eneo lake na
kuwafikisha katika vyombo vya sheria lakini wavamizi hao walirudi tena katika
maeneo hayo na kufanya vitu vya jinai ikiwemo kubaka baadhi ya watu na
kuhatarisha usalama kwa kukata watu mapanga.
Aliiomba
Serikali kuwachukulia hatua kali wavamizi wote wa ardhi katika Kata ya
Mabwepande ili wenye haki waweze kupewa mashamba yao kwa ajili ya kuyaendeleza.
Naye,
Muzamil Karamagi alisema inawezekana wavamizi hao wa ardhi wanalindwa na
wakubwa hivyo aliiomba Serikali kuweka mkakati maalum wa kuwaondoa na kurudisha
ardhi yote kwa wenye hati miliki.
“Kuna
siku tulikuwa na kikao cha wenye mashamba na alikuja Waziri (hakumtaja jina)
lakini kuna kiongozi mmoja aliteremka kwenye meza ya viongozi akaenda kukakaa
na wavamizi na akawapachika jina akawaita wakazi, kitendo kile kilitushangaza
na kutusikitisha mno,” alisema.
Alisema
vitendo kama hivyo vinawavunja moyo wenye haki na wanadhani migogoro ya ardhi
Kata ya Mabwepande inachochewa na baadhi ya vigogo wa Serikali ambao wamevamia
ardhi za watu na wanaziuza kwa watu wengine kinyume cha sheria.
“Ni
jambo la kushangaza umenimilikisha ardhi, mtu mwingine ananivamia ananipeleka
Mahakamani nikamshinda tena sio mara moja inakuwaje sasa wavamizi hawa
waonekane na haki kuliko sisi ambao tunayamiliki maeneo haya kisheria,”
alisema.
Alisema
wavamizi wa ardhi wanaumiza watu kwa maana tangu mwaka 2018 shambani kwake
hajakanyaga na kipindi hicho alipoenda walikuwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na
askari lakini anashanga kuona wavamizi wanaogopwa kuliko wenye haki.
“Serikali
wakati imenipa hati na nalipa kodi ya ardhi kwa mujibu wa sheria mpaka mwaka
huu sina deni, sasa inanisaidiaje kuwaondoa wavamizi katika eneo langu ambalo
Serikali yenyewe ilinipa hati miliki, hawa walioovamia eneo langu wanalindwa na
sheria gani,” alihojia Karamagi.
Naye,
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Mabwepande, Mohamed Tajukhan
Basta alikiri kuwepo kwa wavamizi ya ardhi katika mitaa yote mitano ya Kata ya
Mabwepande ukiwemo mtaa wa Mbopo, Mabwepande, Mji Mpya, Bunju B na Kionzile.
Alisema
wavamizi wa ardhi katika Kata ya Mabwepande ulianza tokea mwaka 2002/2003
ambapo katika Mtaa wake wa Mji Mpya kuna eneo la Serikali linalomilikiwa na
NSSF limevamiwa na wavamizi wa ardhi ambapo ameomba kuwepo maridhiano ili wenye
ardhi na wananchi wakubaliane maeneo yaliyovamiwa yapimwe ili waweze kulipa
kidogokidogo.
“Nilikuwa
na pendekezo kuwa hata hapa katika eneo la Serikali ambalo ni la NSSF kutumike
utaratibu nzuri waliovamia pale ambao tayari wanajua kuwa ni eneo la Serikali
waambiwe kuna mradi aliyekuwa tayari kulipa kwenye utaratibu wa kiserikali basi
apimiwe aendelee na utaratibu na wale ambao wameshindwa basi watakuwa
wameshindwa wenyewe,” alisema.
Kwa
upande wake, Zulfa Sultan ambaye aliuziwa eneo la NSSF alikiri kuuziwa eneo
hilo na wavamizi lakini baada ya kubaini kuwa eneo hilo ni mali ya Serikali
yupo tayari inapopima ardhi katika eneo hilo aweze kufikiriwa kwani yuko tayari
kununua viwanja ili aweze kumilikishwa kihalali.
Kwa
upande wa Valentin Urasa, alisema ni mmiliki halali wa eneo la ekari mbili
ziliziopo Mtaa wa Mbopo Mabwepande ambalo alinunua miaka 12 iliyopita alikuwa
akilima mahindi, mihogo na kulikuwa miembe lakini baada ya miaka mitatu eneo
lake lilivamiwa na alipoulizia kwa majirani aliambiwa kuwa maeneo hayo ni
hatari.
“Baada
ya eneo langu kuvamiwa nilikuja nilikutana na Mzee akaniambia alipigwa mpaka
akavuliwa nguo hivyo nikaona bora nikae mbali nisije kuhatarisha uhai wangu,”
alisema.
Urasa
alisema eneo hilo lina hofu kubwa na wamiliki wa mashamba wanapokwenda
wanaambiwa wawe na tahadhari na hata magari yao wanayaweka mbali kwa kuhofia
usalama hivyo aliiomba Serikali kuwachukulia hatua wavamizi wote wa ardhi.
Bw. Muzamil Mustafa Karamagi, akitoa malalamiko yake.