NA FARIDA SAID,MOROGORO.
UJENZI wa barabara ya Kidatu Ifakara mkoani Morogoro inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 66.9 umefikia asilimia 59,ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi mei 2023.
Barabara hiyo ambayo inategemewa kwa kiasi kikubwa katika usafirishaji wa mazao ya biashara kutoka Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga kwenda Jijiji Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, ambapo kazi kubwa zinazoendelea kwa sasa ni ujenzi wa madaraja likiwemo daraja la mto Ruaha mkuu lenye urefu wa mita 130.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba alisema kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Morogoro Serikali imeona kuna haja ya kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea adha wananchi wanaoitumia barabara hiyo.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo unaendelea kwa kasi ambapo mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anamaliza ujenzi ndani ya muda uliopangwa lengo likuwa ni kuwapunguzia usumbufu wasafirishaji na wafanyabiashara hususani wa mazao.
Alitaja sababu za kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ni pamoja na wingi wa madaraja na makaravati na kusababisha mkandarasi kuongezewa muda wa ujenzi ili aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mang’ula akiwemo Agnes Magesa na Emmanuel Selesius walisema ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kunusuru maisha ya watu hasa wanawake wajawazito na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo.
“Nimefurahi kujengwa kwa barabra hii kiukweli tunamshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hasaan kazi kubwa ameifanya awali tulikuwa tunasafiri masaa matano mpaka sita sehemu ya kwenda masaa mawili.” alisema Bi. Agnes
Barabara ya hiyo inajengwa kupitia ufadhili wa umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza ambapo ujenzi huo pia unahusisha daraja la Mto Ruaha lenye urefu wa mita 130 na madaraja mengine manne.
Kukamilika kwa mradi huo kutaunganisha eneo muhimu la ukuzaji na uzarishaji wa kilimo ukanda wa kusini (southern agricultural growth corridor of Tanzania –SAGCOT )
Pia itarahisisha usafirishaji wa mazao na malighafi kutoka na kwenda bonde la Mto kilombero hususani Wilaya za Kilosa, Kilombero, Ulanga na Malinyi pamoja na maeneo mengine ya mkoa wa Morogoro.