Na Joseph Lyimo
MARA baada ya kuingia nchini kwa janga la maambukizi ya UVIKO-19 mwaka 2020 na kuanza kutolewa kwa chanjo, baadhi ya watu wamekuwa wanadhana potofu na kueneza uvumi kuwa chanjo hiyo inapunguza nguvu za kiume.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya watu wamekuwa na hofu ya jambo hilo, japokuwa wataalamu wa afya wanaeleza mara kwa mara kwamba siyo suala sahihi ni uzushi tuu kwani chanjo ya UVIKO-19 haipunguzi nguvu za kiume.
Mganga wa kituo cha afya Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Tasseni Mbwambo akitoa chanjo ya UVIKO-19 kwa baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, anaeleza kuwa dhana hiyo potofu isiwape hofu kwani chanjo ya UVIKO-19 haina madhara kwa kupunguza nguvu za kiume.
“Baadhi ya watu wanaosema chanjo ya UVIKO-19 inapunguza nguvu za kiume, wanajaribu kupotosha wengine wasipate chanjo kwani hakuna ukweli wa jambo hilo hata kidogo hivyo shirikini bila wasiwasi,” anasema Dkt Mbwambo.
Amesema wataalamu wameshachunguza chanjo hiyo na kuishauri Serikali ikaridhia kuwa hakuna uhalisia wa suala la kupungua kwa nguvu ya kiume pindi mtu akishachanjwa, hivyo ni habari zisizo za kweli.
“Wananchi washiriki kupata chanjo bila kusikiliza maneno ya mitaani yasiyo na maana kwani wanaoeneza dhana hiyo potofu siyo wataalamu wa afya,” anasema Dkt Mbwambo.
Mjumbe wa kituo cha afya cha Mirerani, Mohamed Issa Mughanja anaeleza kuwa wananchi wasipotoshwe na watu ambao siyo wataalamu wa afya wanaozusha maneno yasiyo na msingi juu ya chanjo ya UVIKO-19.
Mughanja anaongeza kwamba suala la chanjo ya UVIKO-19 kupunguza nguvu za kiume ni uzushi wa baadhi ya watu, kwani wataalamu wa afya mara kwa mara wamekuwa wakilifafanua kuwa ni uongo.
“Unamkuta mtu yupo barabarani na hajawahi kupata chanjo ya UVIKO-19 ila anatangaza mambo ambayo hatujui hata ameyapata wapi, ili hali Serikali haiwezi kuwapa kinga ambayo itawaangamiza wananchi wake,” anasema Mughanja.
Mkazi wa kata ya Endiamtu Husna Ally anaeleza kuwa dhana potofu ya chanjo ya UVIKO-19 kupunguza nguvu za kiume ilisababisha mume wake (jina tunalo) kuhofia kuchanja kwa kudhani kuwa atapungukiwa nguvu za kiume.
Husna anaeleza kwamba baada ya yeye kupata chanjo ya UVIKO-19 kwenye kituo cha afya Mirerani, alirudi nyumbani na kumweleza mume wake ili naye akachanje ila akatoa vikwazo.
Anasema iliwabidi waendele kwa wataalamu wa afya waliomueleza yeye na mumewe kuwa hakuna madhara ya kupungukiwa nguvu za kiume ndipo akakubali kupata chanjo.
“Mume wangu alipata chanjo na hivi sasa yupo vizuri tuu hakuna shida nikitaka chakula cha usiku ananipa na yeye akitaka nampa kama ilivyokuwa awali hakuna tatizo lolote,” anasema.
Anaeleza kwamba maudhi madogo yaliyojitokea mara baada ya mume wake kupata chanjo hiyo ni kusikia kichefu chefu na kujisikia homa ila baada ya kumeza vidonge vya kutuliza hali hiyo na kunywa maji alirejea kwenye hali ya kawaida.
Mkazi wa mtaa wa Songambele, Christopher Kimaro anasema kuwa mara nyingi baadhi ya watu wamekuwa na dhana potofu kwa kusambaza habari ambazo hawana uhakika nazo.
“Sisi waswahili ni mahiri mno wa kutangaza jambo baya kulimo mambo mazuri, kwani baadhi ya watu wanatangaza kuwa chanjo ya UVIKO-19 inapunguza nguvu za kiume ilihali hawana ushahidi,” anaeleza Kimaro.
Anasema kwamba Serikali mara kwa mara kupitia wataalamu wa Wizara ya Afya, wamewaelezea wananchi kuwa chanjo hiyo ya UVIKO-19 haipunguzi nguvu za kiume ila baadhi yao bado hawaamini.
Muuzaji magazeti maarufu wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Juma Msangi anasema kwamba yeye binafsi amepata chanjo ya UVIKO-19 na hajapungukiwa na nguvu za kiume.
“Watu waaache kuzusha mambo ambayo hawana uhakika nayo na kusababisha wengine wenye nia ya kupata chanjo hiyo wakarudi nyuma, hii chanjo tunayopata haina madhara ya kupunguza nguvu za kiume hivyo tushiriki kuchanja,” anasema Msangi.
Anasema baada ya yeye kupata chanjo hiyo, amebaini yupo kama awali kwani nguvu zake za kiume hazijapungua hivyo amebaini ni maneno ya watu waliokuwa wanasambaza habari potofu.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, John Victor anasema kuwa yeye binafsi ameshiriki kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ya Jonson Jonson na hakupata tatizo lolote juu ya kupungukiwa na nguvu za kiume.
Hata hivyo, amewataka wanaosambaza taarifa hizo za uongo waachane nazo kuliko kushirikisha chanjo ya UVIKO-19 na upungufu wa nguvu za kiume jambo ambalo siyo la ukweli.
Sheikhe wa mkoa wa Dar es salaam Alhad Salum, amewahi kunukuliwa akizungumza kuwa chanjo ya UVIKO-19 haipunguzi nguvu za kiume kwani hata yeye amechanja na amedhihirisha nyumbani yupo vizuri.
Hivi karibuni, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza jijini Dar es salaam, wakati akihimiza wananchi wapate chanjo ya UVIKO-19 amebainisha kuwa wasiwe na hofu ya chanjo hiyo juu ya kupungua kwa nguvu za kiume, kwani chanjo hiyo haipunguzi nguvu za kiume.