***********************
Na.WAF-Manyara
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Sightsavers Tanzania pamoja na Shirika la Helen Keller International kwa pamoja wamezindua mradi wa miaka miwili wa kutokomeza Vikope(Trakoma) kwa wilaya nne ndani ya Mkoa wa Manyara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na wizara ya afya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (NTD) zimeonyesha tatizo la ugonjwa wa vikope kuwa ni kubwa katika halmashauri za Kiteto,Simanjiro, Babati na Mbulu.
Amesema kuwa tafiti hizo zilionyesha kuwa kuna wagonjwa wanaohitaji huduma za usawazishaji wa vikope ili wasipate upofu wa kudumu takribani 2,441 katika mkoa wa Manyara huku halmashauri ya wilaya ya kiteto ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa 1,768 ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa wagonjwa 403, Halmashauri ya wilaya ya Babati ikiwa na wagonjwa 188 na Halmashauri ya wilaya ya Mbulu ikiwa na wagonjwa 82.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Sightsaver’s Tanzania Bw.Godwin Kabalika amesema kuwa Shirika la Afya Duniani limeweka mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa Vikope unaoitwa “SAFI” Ikiwa na Maana ya S ni Sawazisha,A ni Anza matibabu mapema kwa kutumia Antibiotic, F ni Fanya usafi wa uso na I ni Imarisha usafi wa mazingira hivyo amewaomba wananchi kuzingatia hili ili kuendelea kuwa salama na afya njema ya macho.
Bw. Kabalika amesema mradi huu utahusisha kuwafanyia uchunguzi wa awali wanakaya na watakaobainika kuwa na dalili watafanyiwa uchunguzi wa kina na wataalam wa afya na kupewa matibabu bila malipo kwa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa wa vikope.
Mradi huo unaoenda kutekelezwa kwa miaka miwili uliobeba kauli mbiu ya “EPUKA UPOFU,UGONJWA WA VIKOPE UNATIBIKA,WAHI MATIBABU MAPEMA”unaenda kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan za kuthamini afya za wananchi na kusogeza huduma za afya karibu.