******************
Na Joseph Lyimo
KATIKA kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Manyara wanashiriki kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO-19, viongozi wa Mkoa huo wamejipanga kuhakisha wanatumia ushawishi wa watu maarufu kwenye vijiji na kata kuhamasisha jamii ichanje.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, RC Charles Makongoro Nyerere akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, anasema wamezindua kampeni ya chanjo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii itakayowahusisha watu maarufu wa maeneo hayo.
Amesema miongoni mwa watu maarufu wa maeneo husika watakaotumika kufanya ushawishi wa jamii ni viongozi wa dini, wazee maarufu, viongozi wa kimila na wengineo watakaoongeza kasi ya uchanjaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19.
“Pia tutawatumia wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii katika kuhamasisha kupata wananchi wengi na washiriki kwa wingi ili waweze kupata chanjo ya UVIKO-19,” anaeleza RC Makongoro.
Anasema serikali imekuwa ikitangaza kila wakati kuwa janga la UVIKO-19 bado lipo nchini japokuwa hivi sasa limetulia ila wananchi wanapaswa kupata chanjo ili kujiweka tayari pindi wakipata maambukizi hayo.
“Wataalamu wa afya wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kwani tunataka kuondokana na ile dhana ya kuwa Manyara hatuchanji kwa sababu vifo vya UVIKO-19 vimetokea vichache, sasa hivi tunabadilika,” anaeleza RC Makongoro.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Dkt Aristidy Raphael anasema kuwa mwitikio wa wananchi wa eneo hilo hivi sasa katika kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 ni mkubwa.
Dkt Raphael anasema mara baada ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere kuzungumza na madiwani wa halmashauri nao wakawapa elimu jamii, mwitikio wa kupata chanjo umekuwa mkubwa.
Anasema kwamba madiwani wa halmashauri hiyo walichanja hivyo kuwa mfano kwani kiongozi wa jamii huwezi kusisitiza chanjo ili hali yeye binafsi hajapata chanjo hiyo.
Mmoja kati ya wataalamu wa afya wa kituo cha afya Mirerani Dkt Tasseni Mbwambo anasema kuwa wanawatembelea wananchi mbalimbali wa mji mdogo wa Mirerani katika kuwapatia chanjo ya UVIKO-19.
“Ndugu zangu madereva mnaoendesha pikipiki za kubeba abiria (bodaboda) ninyi mnawabeba watu tofauti ikiwemo wachimbaji madini ya Tanzanite (WanaApolo), wafanyabiashara wa samaki na watu wengine hivyo pateni chanjo,” anasema Dkt Mbwambo.
Anasema wanatoa elimu na kuwapatia chanjo wananchi wa mji huo kwa kuwafuata mahali walipo ili kuhakikisha kuwa wanatoa chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mchungaji wa Kanisa huru la Pentekoste Tanzania (FPCT) Yohana Ole Tiamongoi anasema kuwa jamii imekuwa ikipata chanjo ya UVIKO-19 baada ya kuona kuwa ni hiyari siyo lazima.
“Wananchi wanapewa elimu na kuelezwa kuwa ni hiyari yao kupata chanjo hiyo na wakishatambua umuhimu wake wanashiriki kuchanja,” anasema mchungaji Ole Tiamongoi.
Mmoja kati ya kiongozi wa kimila wa jamii ya wafugaji wa kijiji cha Naisinyai (Laigwanani) Michael Lengitambi anasema kuwa kutokana na janga la UVIKO-19 kutokuwa na dawa, wamekuwa wakiwaeleza wananchi kushiriki chanjo.
“Tumewaeleza wananchi wetu kuwa Serikali haiwezi kutoa chanjo ya UVIKO-19 na jamii ipate matatizo hivyo tumewaeleza jamii ishiriki kupata chanjo hiyo ili kuepukana na maradhi hayo.
Mjumbe wa kamati ya afya wa kituo cha afya Mirerani, Mohamed Issa Mughanja anasema hivi sasa wataalamu wa afya wa eneo hilo wanapita mitaani kutoa elimu kisha kuwapatia chanjo ya UVIKO-19.
“Mwamko ni mkubwa kwa wananchi kwani Mirerani ni mji ambao unaingiliana na watu wa mataifa mbalimbali kutokana na shughuli za uchimbaji, uuzaji na ununuzi wa madini ya Tanzanite,” anaeleza Mughanja.
Amesema hata hivyo, bado watu wachache ambao wanahitaji kupatiwa elimu kutokana na chanjo ya UVIKO-19, kwani elimu ya janga la maradhi hayo bado halijawafikia ipasavyo ndiyo sababu wataalamu wa afya wanawatembelea.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Japhary Matimbwa anasema elimu iliyotolewa kwa wananchi wa eneo hilo na kupitia wataalamu wa afya imesababisha washiriki kupata chanjo.
“Jamii imeona ni aibu kupata UVIKO-19 ili hali chanjo ipo tena inatolewa bila malipo na Serikali, hivyo wameona ni bora wachanje ili hata wakipata maradhi hayo wasipate ugumu wa kupona,” anasema Matimbwa.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt Damas Kayera, anasema hivi sasa kuna mwamko mkubwa kwa wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani 135,000 tayari wamechanja.
Dkt Kayera anaeleza kuwa watu hao 135,000 ni kati ya 669,516 sawa na asilimia 30 wa Halmashauri saba za Wilaya tano za mkkoa huo, ambao wamepatiwa chanjo ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19.
“Hivi sasa wananchi wa mkoa wa Manyara, wamepata mwamko mpya kwani wameshiriki mno katika kupatiwa chanjo ya Uviko-19 tofauti na hapo awali,” anamalizia kwa kusema Dkt Kayera.
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, hadi Julai 3 mwaka huu, Mkoa wa Rukwa ni wa mwisho kwa wananchi wake kupata chanjo ya UVIKO-19 kwa asilimia 10.1, Ruvuma asilimia 46 na Katavi asilimia 33.