*************************
Wakazi wa mji wa Babati Mkoani Manyara wameonekana kufurahishwa na ujenzi wa majengo mapya yanayoendelea kwenye Hospitali ya rufaa ya mkoa wa huo.
Akiongea na Wizara ya Afya mmoja wa wakazi hao Bi. Safia Wakili amesema wananchi wamefurahishwa na ujenzi wa miundombinu hiyo kwani sasa huduma muhimu za uhakika zitaenda kusogezwa kwenye mkoa huo ambapo awali walikua wakizifuata nje ya mkoa.
“Tunamshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan hakika sisi kama wananchi wa Babati na vitongoji vyake tunafurahi sana na matumaini yetu huduma sasa zitakua karibu”. Alisema Safia.
Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Manyara Dkt. Yesige Mutajwaa amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika hospitali hiyo unaendelea vizuri na kwa sasa unafikia hatua za mwisho kukamilika.
“Ujenzi unaoendelea hapa unagharimu kiasi cha bilioni 5 na tunatekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU), ujenzi wa jengo la dharura (EMD), Jengo la Radiolojia, nyumba ya mtumishi pamoja na jengo la Tiba Mtandao (Telemedicine).
“Licha ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi, fedha hizo pia zitanunua vifaa tiba na kugaharamia mafunzo kwa watumishi wetu ili kuboresha huduma katika vitengo vyetu vipya hivyo kuwa na ubora wa huduma”. Aliongeza Dkt. Mutajwaa.